February 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sheria mpya nguzo ya uwekezaji kuongezeka nchini

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline,Katavi.

KITUO cha Uwekezaji Tanzania TIC kimesema idadi ya miradi ya uwekezaji imeongezeka nchini kutokana na usimamizi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutungwa kwa sheria ya mwaka 2022 ambayo imerahisisha na kuondoa vikwazo vingi kwa wawekezaji.

Sheria ya uwekezaji Tanzania, Sheria namba 10 ya mwaka 2022 imeweka masharti ya uwekezaji, masharti ya mazingira bora kwa wawekezaji, mfumo wa kitaasisi kwa ajili ya uratibu, ulinzi, uvutiaji, uhamasishaji na uwezeshaji wa uwekezaji nchini.

Mwenyekiti wa kituo hicho Dkt.Binilith Mahenge Februari 11, 2025, ameweka wazi katika kipindi cha mwaka 2024 miradi 901 ya thamani ya bilioni 9 imesajiliwa ambayo inaongezeko kubwa ukilinganisha na mwaka 2023 miradi 500 ya thamani ya  bilioni 5 imesajiliwa.

Akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoa wa Katavi,Dkt.Mahenge amesema mafanikio hayo yanatokana na ongezeko la uwekezaji, mitaji, miradi na matumizi ya teknolojia mpya jambo ambalo limezalisha  ongezeko la ajira kwa wananchi nchini.

Amesema “Tanzania ina sera madhubuti za uwekezaji zinazolenga kuleta mageuzi katika sekta mbalimbali za kiuchumi. Tunataka kuona wawekezaji wa ndani wakijitokeza kwa wingi na kutumia fursa zilizopo ili kunufaika na mazingira mazuri ya biashara,”

TIC ikiwa na jukumu la kuratibu na kuhamasisha uwekezaji,Dkt.Mahenge ameeleza wana utaratibu wa kutembelea miradi iliyosajiliwa ili kujua changamoto zao na kusikiliza maoni ya wawekezaji, maoni ya mkoa na mkuu wa mkoa kueleza fursa zinazopatikana katika mkoa wake.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko,amesema katika miaka minne ya Rais Dkt.Samia mkoa huo umefunguka kwa kiasi kikubwa kupitia sekta za viwanda, kilimo, madini,ufugaji, misitu na utalii.

Mrindoko amefafanua mkoa wa Katavi kwa sasa unaviwanda 200 hadi 250 vya kuchakata mazao hususani ya mpunga, mahindi na alizeti huku jitihada zinafanyika katika sekta ya utalii kuutangaza zaidi.

Kiongozi huyo wa mkoa ameongeza “ katika sekta ya kilimo ni asilimia 85 hadi 90 wananchi wetu ni wakulima. Madini tunayo na tuna misitu ya asili takribani asilimia 50 ya mkoa ambapo kupitia wilaya ya Tanganyika tunafanya biashara ya hewa ukaa”

Afisa Biashara wa Mkoa wa Katavi Florence Chrisant, amehimiza wawekezaji wengi kujitokeza kwani eneo la mkoa huo bado lina fursa nyingi ambazo bado hazina wawekezaji.

Chrisant amesema wanahitaji viwanda vingi vya kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi  na wawekezaji miundombinu ya usafiri wa kisasa katika ziwa Tanganyika.

Mwenyekiti wa TIC Dkt.Mahenge ametamatisha ziara ya kikazi mkoani Katavi kwa kutembelea kiwanda cha pamba cha NGS kilichopo wilaya ya Tanganyika na kampuni ya Madini Katavi kilichopo halmashauri ya Nsimbo ili kuona tija ya uzalishaji.