Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Lushoto
MBUNGE wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi maarufu Bosnia, amewawezesha viongozi wa kichifu wa kabila la Wasambaa maarufu kama Mazumbe ili waweze kuombea mvua kwa kufanya matambiko ya jadi, huku wakimuomba Mungu.
Shekilindi ameamua kufanya hivyo baada ya kupokea maombi ya wananchi ambao walitaka matambiko ya jadi yarudishwe kama zamani sababu yalikuwa na manufaa makubwa ikiwemo kuombea mvua, na ikanyesha.
Alikutana na baadhi ya Mazumbe hao Machi 6, 2023 mjini Lushoto, na walimueleza mipango yao namna watakavyoombea mvua yenye kheri, na mambo mengine ya kusaidia jamii yao.
Mmoja wa Mazumbe hao, Zumbe Saleh Shebughe kutoka Ubiri alisema mila hizo za jadi zimeshindwa kufanyika kwa muda mrefu sababu zilikuwa na gharama zake ikiwemo wananchi wa eneo husika kuchangia baadhi ya vitu vinavyohitajika ili kufanya shughuli hiyo ya kuombea mvua.
“Wananchi walikuwa wanachangishwa ili kuweza kufanya hilo jambo, lakin kutokana na hali ilivyo ya maisha, wananchi wameshindwa. Hivyo Mbunge amewezesha hilo ili tuweze kufanya kazi ya kuombea mvua, ambapo kwa sisi Wasambaa Wakilindi hili ni suala ambalo tumelifanya kwa miaka mingi.
“Mababu zetu tangu enzi na enzi walikuwa wakienda kuomba mvua kwa kufanya matambiko huku wakimuomba Mungu, baada ya kuondoka eneo hilo, mvua ilikuwa inawafuata nyuma hata kabla ya kufika nyumbani. Hivyo Mbunge kwa kuamua kuendeleza jadi hii ya kufanya tambiko la kuomba mvua, amefanya jambo kubwa la kuisaidia jamii, sababu hali ya ukame inazidi kuwa mbaya kwa kukosa mvua” alisema Zumbe Shebughe.
Shebughe alitaja gharama ya kufanya shughuli hiyo ni kuwa na kondoo watatu, kuku wawili, mkungu wa ndizi na vitu vingine vya kijadi, na shughuli hiyo inakwenda kufanywa mchana kwenye eneo maalumu. Lakini kama shughuli hiyo imeandaliwa kwa muda mrefu, hata ng’ombe anaweza kutumika.
Naye Shekilindi alisema ameamua kuwaunga mkono wananchi kwa kuwawezesha Mazumbe kufanya shughuli hiyo ambayo ni muhimu kwenye jamii ya wananchi wa Wilaya ya Lushoto.
“Nimekuwa na mababu kwenye maisha yangu yote, na wengine maeneo ya kwetu. Hata wakati wa kampeni mwaka 2020, mimi nilikuwa najua changamoto zao, na mojawapo ni kuondoa ukame kwa kufanya matambiko ili mvus inyeshe. Katika kukua kwangu, nimekuwa nikisikia watu wanakwenda kwa Zumbe (Chifu) aweze kuwaondolea shida na matatizo yao kwenye jamii, hivyo siwezi kupuuza jambo hili.
“Nimeona hali ya kiuchumi ya wananchi ni mbaya, na hawana uwezo wa kuchangana fedha ili kununua ng’ombe au kondoo na vitu vingine. Hivyo mimi nimewawezesha sh. 500,000 kwa Mazumbe wa Ubiri, Mlalo na Ngwelo ili wananchi waende kwa Mazumbe na kufanya hilo jambo. Na matambiko hayo ni ya kumuomba Mungu mvua inyeshe yenye baraka, na chakula kitakachopatikana, kisije kikawadhuru wananchi” alisema Shekilindi.
Shekilindi alitoa ushauri kwa wananchi kama Mbunge wao, ifikie hatua Mazumbe hao wasiwe wanakumbukwa wakati wa ukame, bali kuwe na ratiba ya kufanya shughuli zao kabla mambo hayajakuwa magumu kama ilivyo sasa, huku akikubali ushauri wa Mazumbe hao kuwa shughuli hiyo ifanyike kila miezi sita katika maeneo tofauti ya Wilaya ya Lushoto ikiwemo Ubiri, Mlalo, Ngwelo, Bumbuli na Vuga.
Naye Katibu wa Chama cha Tiba Asili Wilaya ya Lushoto Abdallah Mtunguja ‘Manywele’ alisema amepokea kwa mikono miwili kwa jambo hilo lililofanywa na Mbunge kwa kujali matakwa ya wananchi wake, na kuongeza kuwa Mungu anamchagua kiongozi wa kuwasilisha matatizo ya wananchi.
“Vitu kama hivi tumevishuhudia huko nyuma, na kumekuwa na michango inafanywa na kupelekwa kwa Zumbe ikiwemo baadhi ya dawa. Wanaitana siku hiyo wanafanya shughuli, na mwisho wa siku wanaondoka na mvua. Ni jambo limesaidia jamii kwa siku hizo, na tunatakiwa kuliendeza.
“Ushauri watu wananchi na jamii wasipuuze mila na jadi za wazee. Hata Serikali iwathamini Mazumbe (Machifu) na Waganga wa Tiba Asili kama Sheria Namba 23 ya mwaka 2002 ya kuwalinda waganga wa asili” alisema Mtunguja, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Kata ya Lushoto.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa