November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sheikhe,waumini wakumbushwa kumwombea Rais Samia,amani ya nchi

Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

SHEIKH wa Mkoa wa Mwanza, alhaji Sheikhe Hasani Kabeke, amesema Sala ya Eid el Adhaa itafanyika kwenye Uwanja wa Nyamagana na kuwataka Masheikhe na waumini wa Dini ya Kiislamu katika misikiti yao waiombee nchi amani na utulivu na Rais Samia Suluhu Hassan.

Pia amewaasa waumini wa dini hiyo wasikubali kugawanywa na mitizamo ya kiimani ibada mbalimbali iikiwemo sala ya Eid El Adhaa.

Sheikhe Kabeke alitoa kauli hiyo leo,wakati akitoa ufafanuzi kuhusu sala ya Eid el Adhaa amesema kimkoa itaswaliwa kwenye Uwanja wa Nyamagana kesho.


“Wito wangu kwa masheikhe wa misikiti yote na waumini wa Dini ya Kiislamu, waiombee nchi yetu amani na utulivu, wamwombee Rais Samia kwa mazuri anayofanya kwa maendeleo ya nchi na wananchi wake,” amesema Sheikhe Kabeke.

Amesema mambo ya sala ya Eid El Adhaa isiwafanye wagawanyike kwa mitizamo ya kiimani, inaswaliwa kwa kufuata mwandamo wa mwezi, utaratibu ambao ni wa asili badala ya kuswali kwa kufuata watu waliosimama viwanjani.


“Tushikamane na kuijenga dini yetu, tuiombee amani nchi na kujenga utaifa wetu, amani ikikosekana hakuna utulivu.Pia siku ya Eid el Adhaa (siku ya kuchinja) tuchinje na tuwasaidie masikini, yatima,wajane, mafakiri na majirani, tuwape nyama na nyumba zetu zitawaliwe na sauti za Allha Wakbaru (Mwenyzi Mungu Mkubwa),” amesema Sheikhe Kabeke.

Kiongozi huyo wa Dini ya Kiislamu alifafanua wanyama wa kuchinjwa ni ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo ambao hupaswa kuchinjwa baada ya sala ya Eid el Adhaa na siku hiyo waumini wanatakiwa kutokula chochote hadi sala ya hiyo ifanyike.

Sheikhe Kabeke ameeleza kuwa sala hiyo ni mwendelezo wa Suna ya Nabii Ibrahimu ya kutaka kumchinja mwanaye Ismail kabla ya nusura ya Mwenyezi Mungu kuleta kondoo,ingawa imekuwa ikipuuzwa kuwa ni ya watu wa mataifa fulani si sahihi.