January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sheikh Ponda ajitosa sheria ya habari

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam nchini, Sheikh Ponda Issa, ameishauri Serikali kuhakikisha inaweka misingi imara ili tasnia ya habari iepukane na sheria kandamizi.

Sheikh Ponda ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu mchakato wa marekebisho ya sheria ya habari.

Amesema vyombo vya habari vikiwa huru, malengo ya kuanzishwa kwake yatafikiwa.

“Ningekutana na kiongozi wa juu,ningemshauri aweke misingi imara ya kuhakikisha sekta ya habari inapumua kutoka kwenye hayo mazingira kandamizi,”amesema

Aidha Sheikh Ponda amesema vyombo vya habari vikiwa huru vitaweza kuaminika kwa umma.

“Vitasaidia sana katika usambazaji wa elimu mbalimbali inayohitajika katika jamii ambapo vitafikisha kwa namna sahihi na namna ilivyotayarishwa”

“Chombo cha habari kitasaidia sana utawala pamoja na sekta binafsi, vitasaidia kutathimini zile shughuli zao hasa kwa kuandika habari zinazohusu uchumi wao, matakwa ya wananchi, ukosoaji, hivyo chombo cha habari ni kama kioo kwa vyombo vya dola na ni kioo kwa sekta binafsi,” amefafanua Sheikh Ponda.

Aidha Sheikh Ponda amesema mafanikio mengine ya vyombo vya habari nchini kuwa huru ni kuyafanya mataifa ya nje kufahamu ile hali ya taifa lao kwa kufanya uchumi wao uweze kufahamika vizuri.

Kuhusu uhusiano kati ya uhuru wa vyombo vya habari na demokrasia katika nchi, Sheikh Ponda amesema demokrasia inasaidia kuleta amani nchini.