*Akemea lugha za matusi dhidi ya Rais Samia.
*Atoa mfano wa Libya kama somo kwa Watanzania
Na Daud Magesa, Timesmajira Online-Mwanza
SHEIKH wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hassan Kabeke ametoa wito kwa Watanzania, hususan vijana,kuhakikisha wanadumisha amani,mshikamano na kulinda maadili kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
Pia ametoa angalizo juu ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na kauli zinazodhoofisha misingi ya taifa.

Akizungumza baada ya sala ya Eid Al Adha,iliofanyika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza,Sheikh Kabeke amesisitiza umuhimu wa amani,kuheshimu viongozi na kutumia mitandao ya kijamii kwa njia chanya.
“Kukufuru neema ya amani tulionayo na Mungu anakuvisha adhabu,tunapoekelea katika uchuguzi mkuu,maadili yaonekane na amani ya nchi ilindwe, kwa sababu Serikali ya haina dini lakini watu wake wa dini, asitokee mtu anagombea ubunge ama udiwani akapingwa kwa imani ya dini yake (Uislamu ama Ukristo), hata Rais aliyepo madarakani asipimwe kwa Uislamu wake,”amesema Sheikh Kabeke.
Kwa mujibu wa Sheikh Kabeke ,amesema Tanzania imekuwa nchi ya kihistoria kuongozwa na Marais wa dini zote kwa nyakati tofauti,wa kwanza ni Hayati Julius K.Nyerere, wa pili ni Hayati Ali Hassan Mwinyi,Hayati Benjamin W.Mkapa,Jakaya Kikwete na Hayati John Pombe Magufuli,wote waliombewa na waumini wa madhehebu yote.
Hata hivyo amesema, baadhi ya watu wanatumia uhuru wa kujieleza vibaya kwa kumtukana Rais Samia,jambo ambalo halikubaliki kimaadili huku akionya tabia ya kuvituhumu vyombo vya dola bila ushahidi wa kutosha kuhusu masuala ya utekaji.
“Wanaotoa tuhuma watoe suluhisho,kushutumu pekee haitoshi, wanayo fursa ya kushauri na kusaidia taifa kufikiria maridhiano na maendeleo,”amesema.
Hata hivyo, Sheikh Kabeke amewaagiza waumini wa kiislamu katika misikiti yote kufunga ili kumwombea Rais Samia na uchaguzi mkuu na nchi ivuke salama ambapo amesema watasoma albadir 4444 (Sura Yasin)dhidi ya wanaomwombea mabaya Rais.
Pia,Sheikh Kabeke amewaonya vijana wa Kiislamu wanaotumia mitandao ya kijamii vibaya kwa kupandikiza chuki,migawanyiko ya imani au kisiasa kwani wanauchafua Uislamu.

Huku akitolea mfano wa Libya,ambako machafuko ya kisiasa yaliyoanza kwa maneno na migawanyiko mitandaoni hatimaye yaligeuka kuwa janga la kitaifa,”Leo hii Walibya wanamkumbuka Hayati Kanali Muammar Gaddafi, lakini ni baada ya kuona machungu ya kuvurugika kwa taifa lao,tujifunze kutoka kwao,”.
Amehimiza wananchi kushiriki uchaguzi kwa amani, kufuata sheria na kuepuka kuchochewa na propaganda za kugawa huku akiviasa vyama vya siasa kutenda haki kwa mchakato wa mchujo ikijumuisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kutenda haki kwa vyama vyote.
More Stories
Kiongozi wa Mwenge awataka RUWASA kukamilisha mradi wa maji kwa wakati Kilindi
Balozi Nchimbi aongoza waombolezaji kumuaga Mzee Mongella
Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua mama yake mzazi