December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sharif awataka Waislam kutumia mwezi wa Ramadhani kuchuma yalio mema

Na Heri Shaaban, TimesMajira Online

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi (CCM)Kata ya Ilala Sabry Abdalah Sharif, awataka waumini wa dini ya kiislam kutumia mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa ajili ya kuchuma yale yalio mema ambayo tunaelekezwa na Mwenyezi Mungu.

Mwenyekiti wa Wazazi Sabry Abdalah Sharif, alisema hayo katika mashindano ya pili ya kuifadhi Qurani tukufu yaliyofanyika Nyeburu Kata ya Buyuni ambapo Sabry alimwakilisha Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Ilala Mohamed Msophe .

“Waumini wezangu wa dini ya Kiislam tutumie mwezi wa Ramadhani kwa ajili ya kufanya mema ambayo tunaelekezwa na dini yetu ya kiislam na kuchukia matendo mabaya ambayo yanaenda kinyume na dini yetu hivyo tuzidishe ibada na kuchuma yalio mema “alisema Sabry

Mwenyekiti Sabry Sharif aliwataka waumini wa dini hiyo kufunga na kufanya ibada ili funga yao iweze kukamilika,alitumia fursa hiyo kumpongeza Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Buyuni Hamis Gea , kwa kuratibu mashindano hayo kila mwaka kwa ajili ya kuwajengea misingi ya dini ya kiislam watoto kila wakati wamkumbuke Mwenyezi Mungu.

Katika mashindano hayo ya kuifadhi Qurani tukufu mwaka huu 2024 mshindi wa kwanza Fatuma Shaibu kutoka Kigezi alijinyakulia shilingi 70,000/=

Wakati huo huo Mwenyekiti Sabry alizungumzia mmomonyoko wa maadili kwa vijana aliwataka Wazazi kuwalea watoto katika misingi mema dini wasiingie katika mmomonyoko wa maadili.

Alisema Wazazi wana jukumu kubwa la kuwalea watoto wao kwa misingi ya kufuata dini yao ili wasiingie katika mmomonyoko wa maadili.

Aidha aliwataka Wazazi wa Nyeburu kushirikiana na Jumuiya ya Wazazi ya CCM katika kulea watoto katika misingi bora kwani jumuiya ya Wazazi itasimamia sekta ya Elimu, Malezi na Mazingira.

Alitumia fursa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza sekta ya Elimu na Afya ambapo ametoa pesa nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo na miundombinu ya Barabara.