March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali,NYANZAGA Mining wasaini makubaliano ya nyongeza uchimbaji madini

*Mradi  utakaogharimu zaidi ya tirioni 1

*Ni mgodi wa dhahabu uliopo Sengerema mkoani Mwanza 

*Mavunde aeleza kuwa utachochea ukuaji wa uchumi wa nchi

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza 

Serikali  ya Tanzania na kampuni ya uchimbaji madini  NYANZAGA (NYANZAGA Mining Limited) imesaini mkataba wa  makubaliano ya nyongeza kwa ajili ya mradi wa  uchimbaji mkubwa wa madini ya dhahabu  kupitia kampuni ya ubia ya Sotta Mining Corporation Limited,ambao unaelezwa kuwa kichocheo cha uchumi wa taifa na ustawi wa wananchi.

Utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa dhahabu katika mgodi wa Nyanzaga,uliopo Kata ya Igalula wilayani Sengerema mkoani Mwanza.  unatekelezwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Perseus Mining Limited kupitia kampuni ya NYANZAGA Mining Company Ltd,unaotarajia  kuwa kichocheo  cha ukuaji wa uchumi wa taifa na ustawi wa wananchi katika kipindi chote cha utekelezaji wake.

Waziri wa Madini Anthony Mavunde( kushoto) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Perseus Lee-Anne de Bruin ( kulia)wakisaini mkataba kati Serikali ya Tanzania na kampuni ya uchimbaji madini NYANZAGA (NYANZAGA Mining Limited)  wa makubaliano ya nyongeza kwa ajili ya mradi wa uchimbaji mkubwa wa madini ya dhahabu kupitia kampuni ya ubia ya Sotta Mining Corporation Limited,halfa iliofanyika Agosti 20,2025, katika eneo la mradi Kata ya Igalula wilayani Sengerema mkoani MWanza

Akizungumza Agosti 20,2025,wilayani Sengerema katika hafla ya utiaji saini ,Waziri wa Madini Anthony Mavunde,amesema kutokana na Wizara kuanzisha timu ya majadiliano, katika mkataba huo umiliki wa hisa za Serikali zimepanda kutoka asilimia 16 hadi asilimia 20 huku mbia huyo akiwa na asilimia 80.

Mavunde amesema,uwekezaji huo ni wa zaidi ya tirioni moja na taarifa ya awali ya utafiti unaonesha ya kwamba maisha ya mgodi huo utakuwa ni miaka 12 mpaka 15, ingawa utafiti   bado unaendelea huku akisisitiza kuwa  wananchi watapata mafanikio na kunufaika kupitia   mgodi huo kwa  muda wote huo.

“Mradi kama huu ni watu wamekuja kuomba leseni ya utafiti wizarani,wametumia gharama zao,wameleta mtaji wao.Serikali ina kwenda kupata asilimia 20 bila kuchangia senti moja,pia tuna kodi,tozo na ushuru mbalimbali,tunakwenda kunufaika na uwekezaji  huu ikiwemo  wananchi wa eneo hili na taifa kwa ujumla kwa kutoa fursa za ajira,kukuza pato la Halmashauri ya Sengerema,Mkoa wa Mwanza pamoja na taifa kwa ujumla,”amesema Mavunde.

Pia amesema  Serikali imeweka mkazo  kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu kupitia utoaji wa huduma na bidhaa mbalimbali zinazohitajika kwenye mradi huku kampuni hiyo italazimika kushirikiana na jamii  kuboresha huduma za kijamii kama shule, afya, maji na miundombinu pamoja na kusaidia miradi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.

Sanjari na hayo Mavunde,amesema anatambua kazi zinaendelea  ikiwemo ujenzi wa  nyumba 262 za wale walioguswa na mradi na tayari nyumba 129 zimekamilika huku idadi kubwa ya  wananchi  wameisha hamia kwenye nyumba hizo.

“Naitaka kampuni ya Sotta Mining Corporation Limited kuhakikisha kuwa kama mlivyosema Oktoba 31,2025, zoezi ya ujenzi wa nyumba liwe limekamilika  na wananchi wote waliopisha mradi waweze kukabidhiwa nyumba zao  ili waendelee na maisha yao,”.

Aidha Mavunde ameeleza kuwa kampuni ya Sotta Mining imerudisha leseni yake Serikalini, na Wizara itahakikisha leseni hizo zinagawiwa kwa wananchi wa Wilaya ya Sengerema, huku akihimiza kampuni  kuendelea kutoa msaada wa kiufundi kwa wachimbaji wadogo.Pia  ameliagiza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kupeleka mtambo maalum wa kuchoronga (drilling rig) ili kusaidia wachimbaji wadogo kuongeza tija.

Waziri wa Madini Anthony Mavunde( kushoto) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Perseus Lee-Anne de Bruin (katikati)wakipeana mikono  huku wakiwa wameshika  mkataba baada ya kusaini ,mkataba huo ni kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya uchimbaji madini NYANZAGA (NYANZAGA Mining Limited) wa makubaliano ya nyongeza kwa ajili ya mradi wa uchimbaji mkubwa wa madini ya dhahabu kupitia kampuni ya ubia ya Sotta Mining Corporation Limited,halfa iliofanyika Agosti 20,2025, katika eneo la mradi Kata ya Igalula wilayani Sengerema mkoani Mwanza

Mkurugenzi wa Kampuni ya Perseus  Lee-Anne de Bruin ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kufanikisha mazungumzo hayo na hatimaye kusainiwa mkataba huo wa nyongeza kati ya Serikali na kampuni yao ambapo utaruhusu shughuli za uzalishaji kuanza pindi shughuli za ujenzi zitakapokamilika mwanzoni mwa mwaka 2027.

“Mradi huu utaleta manufaa  kwa taifa hili mara baada ya kuanza uzalishaji, na tunatarajia dhahabu ya kwanza kuzalishwa robo ya kwanza ya mwaka 2027,Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza  uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliosaidia kurahisisha mchakato wa uwekezaji huu mkubwa,” amesema  Lee-Anne.

Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu,amesema kupitia  mgodi huo taifa litapata maendeleo endelevu na faida zaidi kwani ni moja ya miradi mikubwa zaidi ya madini Tanzania,ambao unatarajia kuiingizia Serikali kiasi cha bilioni 400 lakini pia mapato kupitia kodi, gawio na vitu vingine pamoja na kutoa fursa ya  ajira kwa wananchi.

“Mradi huu utaimarisha uchumi wetu, katika kipindi cha mnyukano wa uchumi duniani, kilichotusaidia ni madini, ni bidhaa inayotuletea fedha nyingi  za kigeni na kusaidia kuimarisha uchumi wetu,”amesisitiza Mchechu.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,  Said Mtanda ameeleza kuwa kiasi cha  cha dola za Marekani milioni 500,ambazo  zitakazotumika kujenga mradi huo, zitasaidia kubadilisha Mkoa mapato kuongezeka. 

Waziri wa Madini Anthony Mavunde akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano ya nyongeza kati Serikali ya Tanzania na kampuni ya uchimbaji madini NYANZAGA (NYANZAGA Mining Limited),kwa ajili ya mradi wa uchimbaji mkubwa wa madini ya dhahabu kupitia kampuni ya ubia ya Sotta Mining Corporation Limited.Hafla liofanyika Agosti 20,2025, katika eneo la mradi Kata ya Igalula wilayani Sengerema mkoani Mwanza