December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yazidi kupata imani kubwa na TBS kwa kubadilika kiutendaji

Na Reuben Kagaruki,TimesMajira,Online Dar

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Geofrey Mwambe amesema wameridhishwa jinsi Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilivyojipanga kufanikisha biashara kutokana na jinsi shirika hilo lilivyobadilika kiutendaji na hivyo wao wanapata imani kubwa kama viongozi wa Serikali.

Waziri Mwambe akiwa ameoongozana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo,Exaud Kigahe, alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana alipofanya ziara katika shirika hilo na kufanya mazungumzo na menejimenti kisha kuwa na mkutano na wafanyakazi.

Amesema pamoja na kubadilika kwa shirika hilo, wanatamani waone TBS ni kimbilio la wajasiriamali, ambayo inawafuata kule walipo na wanakuwa na TBS ambayo inaanda na kusajili viwango ndani ya muda mfupi zaidi.

Waziri Mwambe amesema wamekubaliana na menejimenti ya shirika hilo kutengeneza mpango ambao utawezesha uandaaji wa kiwango cha chini kabisa ufanyike ndani ya miezi mitatu.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Geofrey Mwambe (katikati) na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe (kushoto) wakiwa kwenye kikao na menejimenti na uongozi wa Shirika ya Viwango Tanzania (TBS) ikiwa ni kikao cha kwanza na Taasisi hiyo tangu walipoteuliwa kuwa mawaziri wa Wizara hiyo. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Yusuf Ngenya. Kikao hicho kimefanyika jana Ubungo – Dar es salaam.

“Tumeambiwa muda wa chini sana wa kuandaa kiwango ni miezi sita, kwa sababu kinaandaliwa hadi kutangazwa katika gazeti la Serikali, kupata maoni ya wadau hadi kuidhinishwa kuwa sheria, kwa hiyo tumekubaliana maeneo yale ambayo yanagusa TBS na hata wizara nyingine sisi tutaangaika nayo ili kuhakikisha muda wa uandaaji wa viwango unatoka miezi sita hadi mitatu na uandaaji wa kiwango cha juu ushuke hadi miezi tisa kulingana na aina bidhaa,” ameagiza Waziri Mwambe.

Amesema Wizara ya Viwanda na Biashara na TBS wakiwa ni wasimamizi wa biashara wanataka kuona ufanikishaji biashara unarahisishwa ili kupata wafanyabiashara wengi zaidi pamoja na walipa kodi.

Kwa mujibu wa waziri huyo hatua hiyo itasaidia kupatikana hapa nchi bidhaa ambazo zinaagizwa nje ya nchi kwa kutumia fedha za kigeni.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Geofrey Mwambe na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe wakiwa wameambatana na Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Athuman Ngenya wakisikiliza maelezo kutoka Mkuu wa Maabara ya kemia, Charles Batakanwa wakati wakikagua maabara za TBS jana Ubungo Dar es Salaam.

“Kwa hiyo tumeona namna ambavyo TBS inaweza kuwa sehemu nzuri zaidi ya kufanikisha biashara na kusaidia viwanda vyetu kukua,”amesema Waziri Mwambe na kuongeza;

“Na tumefurahi kuona namna shirika lilivyojipanga na sisi tumetoa maelekezo katika baadhi ya maeneo hususani ya wao (TBS) kutoka nje na kwenda kuwafuata wenye viwanda pamoja na wajasiriamali na siyo kuwasubiri ofisini.”

Aidha, Waziri Mwambe ameagiza shirika hilo kuandaa muongozo wa ukaguzi wa bidhaa bandarini na katika vituo vyote vya mipakani kwa kushirikiana na taasisi zingine ambazo zipo chini ya wizara nyingine.

“Kuna vitendo vya watumishi wa Serikali ambao wapo kwenye vituo hivyo kutofanya ukaguzi kwa pamoja.

Kila mtu anataka afanye peke yake ili apate nafasi ya kuongea na mwenye mzigo ili ikiwezekana avute pesa pale kama rushwa, kwa hiyo tumemuambia Mkurugenzi Mkuu wa TBS (Dkt. Yusuf Ngenya) kwenda kusimamia ukaguzi wa pamoja wa bidhaa na taasisi ambayo itaonekana wao hawataki basi sisi tupate taarifa ili mimi niongee na waziri mwenzagu ambaye ile taasisi ipo chini yake,”ameagiza Waziri Mwambe.

Kwa mujibu wa Waziri Mwambe lengo la hatua hiyo ni kutaka kupunguza muda wa mizigo kukaa bandarini na kwenye vituo vya ukaguzi mpakani pamoja na kuondoa rushwa kwenye ukaguzi wa mizigo.

Mkuu wa Maabara ya Kemia katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mhandisi Charles Batakanwa (kulia), akitoa maelezo kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Geofrey Mwambe (kushoto) kuhusu maabara hiyo inavyofanyakazi alipofanya ziara makao makuu ya shirika hilo juzi, jijini Dar es Salaam.

Ametaja eneo lingine ambalo walikubaliana na menejimenti ya shirika ni TBS kuendelea kubaki alama ya kufanikisha biashara kimataifa, kuandaa viwango haraka na wanataka wajasiriamali kwenye kanda mbalimbali nchini waweze kuhudumiwa kwa kufikiwa, kwani wanachokitaka ni uchumi wa viwanda na viwanda haviwezi kuota ghafla.

“Kwa hiyo ni lazima turuhusu wajasiriamali wadogo wadogo wakue kwa wao kufanya shughuli zao kwenye maeneo tofauti. Tumewaambia TBS, SIDO na NEMC waweze kutoa miongozo ni namna gani mjasiriamali mdogo anaweza kuanza kuchakata bidhaa hata kama wakiwa majumbani au sehemu zisizo rasimi, lakini kwa utaratibu ambao umeelekezwa na TBS pamoja na SIDO,” amesema Waziri Mwambe na kuongeza;

“Wakizingatia hayo itakuwa ni rahisi mno kupata bidhaa ambazo hazijachafuliwa na ikawa ni rahisi kwa TBS kuwapa alama yao ya ubora.”

Ametaja eneo lingine ambalo amesisitiza kwenye ziara hilo kuwa ni uadilifu. “Unaweza kuwa mwepesi kwenye kazi, lakini kama unapokea rushwa na kutoa matokeo ya maabara ambayo sio sahihi wewe haufai, kwa hiyo tumeongea na uongozi wa TBS na watumishi wao kuhakikisha wanazingatia maadili ya utumishi wa umma,” amesisitiza.

Amesema matokeo ya maabara yanaaminika na kwa bahati nzuri kati ya maabara tisa za shirika hilo, saba zimepata cheti cha ithibati kutoka taasisi zinazotambulika kimataifa ikiwemo za SADC, hivyo matokeo yake yanakubalika dunia nzima.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Geofrey Mwambe (katikati) na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara akiongea na wafanyakazi wa Shirika ya Viwango Tanzania (TBS) ikiwa ni kikao cha kwanza na Taasisi hiyo tangu kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara hiyo, Ubungo – Dar es Salaam.

“Kwa hiyo matokeo yanapokuwa ya hovyo kwa sababu umepokea rushwa maana yake unapotosha dunia nzima, kwa hiyo hatutaki TBS na Tanzania nzima tukashushwa kwenye kiwango cha kuaminiwa. Tunahitaji kuwa na kiwango cha juu cha uaminifu kwa wafanyakazi,” amesisitiza.

Suala lingine ambalo Waziri huyo aligusia kwa TBS na taasisi zingine ni kuwa na mawazo ya kibiashara, kwani Rais John Magufuli anaangaika kujenga uchumi, hivyo wanahitaji kutengeneza wigo wa walipa kodi wengi ili waweze kukusanya kodi za kutosha.

Amesema watu wengi wapo mitaani wanatafuta ajira hivyo kama kutakuwa na biashara nyingine na vijana wengi wakaingia kwenye shughuli za biashara hawatakuwa na presha kubwa ya ajira kwa vijana na kwamba watatengeneza fedha nyingi za kigeni kwa kuzalisha bidhaa ambazo mara nyingi zinaagizwa kutoka nje.

Wazuri Mwambe (kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa mtaalam wa maabara ya ngizi na nguo

“Kwa hiyo tunataka TBS wajione wana wajibu wa kukaa zaidi kibiashara ili kila mmoja aweze kuwezeshwa kufanya biashara zaidi,” amesema.