December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yazidi kuahidi neema kwa wafanyabiashara

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

WIZARA ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara imesema inaendelea na jitihada za kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kuendelea na utekelezaji wa Mpango wa Kuimarisha Mazingira ya Biashara nchini (MKUMBI) na kuboresha upatikanaji wa miundombinu na huduma wezeshi kama vile gesi asilia, ujenzi wa reli, barabara, viwanja vya ndege, bandari, umeme, maji na ardhi kwa uwekezaji.

Hayo aliyasema jana jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo,Ally Gugu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Mkutano wa Majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi utakaofanyika Februari 2, 2023.

Mkutano huo utaandaliwa na Wizara hiyo kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na wadau wa Sekta ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Alisema hatua ya kuandaliwa kwa mkutano kunaakisi dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukuza na kuimarisha majadiliano na ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi

Mkutano huu unaotarajia kufanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam mgeni rasmi na mzungumzaji mkuu anatarajiwa kuwa Dkt. Ashatu Kijaji na uhudhuriwa na washiriki zaidi ya 500.

Amesema unalenga kufanya majadiliano ya namna ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kwa lengo la kukuza uchumi na kuchochea maendeleo ya Taifa.

“Mkutano huo utakua na washiriki zaidi ya 500 ukijumuisha viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo viongozi wakuu kutoka Serikali ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mawaziri wa kisekta, makatibu wakuu wa wizara za kisekta, wenyeviti wa kongani mbalimbali, wamiliki wa kampuni, wamiliki wa viwanda, vyama vya sekta binafsi, jumuiya za wafanyabiashara, wawekezaji, wafanyabiashara wadogo na wa kati, wakuu wa taasisi za serikali, watafiti wabobezi, watunga sera, washirika wa maendeleo na Asasi za Kiraia (AZAKI).”

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Godwill Wanga amesema suala zima la uboreshaji mazingira ya biashara ni la umuhimu kwani kwa sasa uchumi wa nchi upo katika asilimia 5.2 ambapo lengo ni kufikia asilimia 8.

“Uchumi unapokua kuna faida kubwa sana kwa mtu mmoja mmoja lakini pia kwa nchi yenyewe hivyo ni vyema kuboresha mazingira ya biashara kwa njia mbalimbali ili kuweze kufika pale tulipokusudia.” alisema Wanga.

Naye Mkurugenzi wa Bodi Kutoka TPSF, Octavian Mshiu amesema Tanzania ni moja ya nchi 10 za Afrika ambazo mazingira yake ya biashara yamebireshwa kutokana na uongozi mahiri wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia.

“Tupo bega kwa bega na Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia katika kushirikiana na serikali kwenye mijadala kama hiyo,” alisema na kuongeza kwamba;

“Tangu Rais ameingia madarakani, ameboresha mazingira ya biashara hilo si kwamba linatambulika kitaifa bali linatambulika kidunia.”