Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga
SERIKALI imezindua mwongozo wa taifa wa kutoa matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya utakao toa fursa za matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya nchini ambapo matarajio ni kufika mwisho mwaka kuwe na vituo 6 vya huduma ya methadone.
Akizindua mwongozo huo wakati wa uzinduzi wa huduma ya methadone mkoani Tanga, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia,Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuwa mwongozo huo umetengenezwa kwa ushirikiano wa Wizara pamoja na shirika la MDH.
Tanzania inakadiriwa kuwa na jumla ya waathirika wa dawa za kulevya kati ya watu 200,000 hadi 350,000 kwa mujibu wa takwimu za wizara ya afya.
Akitoa takwimu hizo Waziri Ummy amesema kuwa kati yao waathirika takribani 30,000 wanatumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga huku kukiwa na makadirio ya asilimia 35% ya kiwango cha maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwenye jamii ya waathirika hao.
Amesema kuwa kiwango hicho ni kikubwa karibu mara tano zaidi ya kiwango cha maambukizi kwenye jamii hiyo kwa mwaka 2014.
Sambamba na hayo, hali ya maambukizi mapya katika kundi hilo kwa sasa yamepungua hadi kufikia mdungaji mmoja katika kila wanaojidunga 10 ikilinganishwa na wanaojidunga 4 kati ya 10 kwa mwaka 2014.
“Utafiti iliyofanyika mwaka 2016 unaonyesha kuwa Mkoa wa Tanga una zaidi ya waathirika 5,190 na hivyo kuufanya mkoa huo kuwa wa pili nchini kwa kiwango cha maambukizi” amesema Waziri Ummy.
“Mkoa wa Tanga unaidadi kubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya hali inayosababisha ongezeko la watumiaji kutokana na uwepo wa mazingira chochezi ya utumiaji tofauti na mikoa mingine hapa nchini,” amesema Ummy.
Ameongeza kuwa kutokana na changamoto hiyo, serikali iliamua kuja na tiba ya bure ya dawa ya methadone kwa ajili ya kuwahakikishia tiba waathirika wa dawa za kulevya.
“Lengo la serikali ni kufungua vituo sita katika maeneo yenye viwango vikubwa vya maambukizi, ili kufika mwisho wa mwaka 2020 serikali itakuwa imesogeza huduma hiyo karibu na wananchi” amebainisha Waziri Ummy.
Naye Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, James Kaji amesema kuwa uwepo wa kituo hicho ni mpango wa kufikisha huduma kwa walengwa kwa haraka.
Amesema kuwa ufunguzi wa kituo hicho ni muendelezo wa uwepo wa vituo nane ambavyo tayari vinatoa huduma kila siku kwa waraibu wapatao 8,500 kila siku.
Hata hivyo Kaji ameishukuru serikali kwa kuja na mtaala wa athari za dawa za kulevya ambao utaanza kutumika mashuleni kuanzia darasa la tatu hadi sekondari ambao utasaidia kutoa elimu ya janga hilo.
Mkurugenzi wa Shirika la Amref Dkt Florence Temu amesema kuwa Shirika hilo limeamua kuunga mkono jitihada za serikali kupambana na ugonjwa huo kwa kuanzia na uanzishwaji wa kituo cha muda ambacho kimegharimu kiasi cha shilingi milioni 14.
Amesema “uwepo wa huduma hiyo utasaidia jamii ya Wanatanga wanaohitaji huduma hiyo kwa kiasi kikubwa.”
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Jonathan Budemu amesema hadi kukamilika jengo hilo, serikali inatarajia kutumia kiasi cha shilingi milioni 786. Amewaomba wananchi pamoja na wadau wengine kuwashawishi waathirika wa dawa za kulevya kufika katika kituo hicho kwa ajili ya kupata huduma za tiba na ushauri
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari