July 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yawahakikishia umeme Vijiji vya Manzwagi, Kidunyashi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

NAIBU Waziri wa Nishati. Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea kuwasimamia kwa umakini wakandarasi ili waweze kukamilisha kazi zao kwa wakati na kwa ufanisi, pia amewaelekeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha wanaongeza nguzo 40 ambazo ni Sawa na kilometa mbili kwa wananchi wa vijiji vya Manzwagi na Kidunyashi kabla ya tarehe 27 Julai, 2024.

Kapinga amesema hayo tarehe 03 Julai, 2024 alipokuwa anahitimisha ziara yake katika Wilaya ya Kahama kwenye Vijiji vya Manzwagi na Kidunyashi vilivyopo Wilaya ya Kahama Mjini Mkoani Shinyanga.

Kapinga amesema Vijiji hivyo vitafikiwa na Nishati ya Umeme mwezi huu wa julai 2024 ambapo kijiji cha Manzwagi kitapata umeme ifikapo tarehe 14 julai na kijiji cha Kidunyashi kitapatiwa umeme ifikapo tarehe 10 julai, 2024.

Amesema kutokana na suala la maendeleo kuwa ni hatua, Serikali iliweka nguvu kubwa katika usambazaji wa umeme vijijini na sasa hatua inayofuata ni kupeleka umeme vitongojini ili kuwezesha shughuli za kijamii na kiuchumi.

“Nawashukuru REA wamesema watawafikishia umeme watu wa Manzwagi tarehe 14 julai 2024 niwatowe hofu wananchi wa Manzwagi kuwa umeme utawafikia Ndani ya siku zilizopangwa na pia tutawaongozea Nguzo nyingine 40 ili umeme uweze kufika Vijiji vyote,” Amesema Kapinga.

Vilevile Kapinga Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inafanya Miradi mingi sana kwenye upande wa uzalizaji, usafirishaji na usambazaji wa Umeme Na Fedha nyingi zimetengwa kwenye uzalishaji wa Umeme.

“Mradi Mkubwa Wa Julius Nyerere (JNHPP) unaozalisha Megawati 2.115 umegharimu zaidi ya trilioni 6 ambapo mradi huu mkubwa utatufanya tuweze kuzalisha umeme zaidi ya huu tunaoutumia sasa” ameeleza kapinga.

Naibu Waziri Kapinga ametoa wito kwa Wananchi kuhakikisha wanailinda miundombinu ya umeme ili iweze kutumika kwa muda mrefu.

“Niwaombe Wananchi tutunze miundombinu hii ya umeme ili iweze kutumika kwa muda mrefu pamoja na kutuletea tija katika shughuli zetu za Maendeleo” Amesisitiza Kapinga.

Aidha kuhusu bei ya umeme, Kapinga ameongeza kuwa atakaa na REA na kufanya tathimini bei ya kuunganisha  ya 320,000 au 27,000.

“Tutafanya Tathimini suala hili ili tuweze kuona namna ambavyo itawafanya Wananchi waweze kuunganishiwa umeme kwa Bei ya Elfu 27 ni yetu ni kuhakikisha Mwananchi anafikishiwa huduma ndani ya Eneo lake”

Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro  ameshukuru kazi kubwa ya usambazaji umeme inayofanywa katika maeneo mbalimbali na pia amempongeza Mbunge wa Kahama Mjini Jumanne Kishimba kwa kuwajali Wananchi kwa kuwapatia Maendeleo kwa wakati.