November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yawaasa vijana kutambua na kuthamini vipaji vyao

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amewaasa vijana nchini kutambua na kuthamini vipaji vyao ili waweze kufikia malengo waliojiwekea na kuleta tija kwenye jamii inayowazunguka.

Naibu Waziri Katambi amesema Julai 23, 2022 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Taasisi ya Mzalendo Project Foundation iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Jijini Dar es Salaam.

Alieleza kuwa, azma ya Serikali ni kuendelea kuwajengea vijana mazingira wezeshi yatakayo wapatia fursa mbalimbali zitakazo wawezesha kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ipo tayari wakati wote kutoa msaada wa hali na mali utakao hakikisha vijana wanapata fursa za ajira na upatikanaji wa mitaji itakayo wawezesha kujishughulisha na kazi ambazo zitaweza kuwaingizia kipato,” alisema Katambi

Aidha, Naibu Waziri Katambi alielezea mikakati ya Serikali katika kusaidia vijana ikiwa ni pamoja na tafiti zilizofanyika kwa lengo la kuangalia namna nzuri ya kupunguza changamoto ya ajira. Pia amefafanua hatua zilizochukuliwa katika kuboresha Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007.

Vile vile, ameelezea hatua zilizochukuliwa na serikali kuhusu mabadiliko ya mitaala ili iendane na uzalishaji wa fursa nyingi za ajira na kuuwasaidia vijana kujiajiri zaidi sambamba na kupata ujuzi na maarifa ya kukabiliana na changamoto za ajira.

Aidha, Naibu Waziri Katambi amepongeza vijana nchini kwa namna wanavyojitoa na kujenga uthubutu wa kufanikisha malengo yao, hivyo amewataka vijana kutambua na kuthamini vipaji vyao ili waweze kutimiza ndoto na malengo yao kwa ustawi wa Taifa lao.

Akizungumza awali, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mzalendo Project Foundation (MZPF), Bw. Enock Mwesiga alisema kuwa lengo la taasisi hiyo ni kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wa Vyuo vikuu nchini mara baada ya kumaliza elimu yao ya juu, Pamoja na kusaidia vijana kupata ufadhili wa kifedha kutoka taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi ili waweze kutimiza malengo ya mawazo yao ya kijasiriamali na kusaidia jamii na taifa kwa ujumla.

“Taasisi hii ya Mzalendo Project Foundation imekusudia kutoa mafunzo ya kijasiriamali kwa vijana hususan wa elimu ya juu nchini ili waweze kuepukana na suala la utegemezi wa ajira za Serikali badala yake waweze kujiajiri na kuajiri wenzao,” alieleza

Naye, Msanii wa Kizazi Kipya Kala Jeremiah, ameeleza kuguswa na vijana hao ambao wameonyesha uthubutu kwa kuanzisha taasisi hiyo. Hali kadhalika msanii huyo alitoa wito kwa vijana kuthamini muda ili waweze kuambatanisha vyema ndoto zao na malengo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi ameshiriki katika Kongamano la Sensa na Uchumi lililoandaliwa na MAYODA Economic Development Group ambalo limelenga kuongeza mwamko kwa kutengeneza mabalozi wengi ili kuongeza chachu kwa wananchi kujitokeza kuhesabiwa.

Akiwa katika kongamano hilo, Naibu Waziri Katambi amehamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23, 2022.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi akipokea tuzo kwa niaba ya Mhe. Rais, Samia Suluhu Hassan ikiwa ni pongezi ya kuthamini mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa katika Kongamano la Sensa na Uchumi lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere International Convention Centre. Wa tatu kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa MAYODA Economic Development Group, Bw. Agustino Matefu akikabidhi tuzo hiyo.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mzalendo Project Foundation (MZPF), Bw. Enock Mwesiga (kulia) wakati wa hafla ya taasisi hiyo uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Jijini Dar es Salaam Julai 23, 2022.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na vijana wakati wa hafla ya uzinduzi wa Taasisi ya Mzalendo Project Foundation iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Jijini Dar es Salaam.
 
Sehemu ya vijana wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) wakisikiliza maelezo ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi wakati wa hafla hiyo.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi (wa pili kutoka kushoto) akikabidhiwa zawadi ya picha iliyochorwa ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS). Kushoto ni Mlezi wa Chuo hicho, Bi. Stella Jackson. Kulia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mzalendo Project Foundation (MZPF), Bw. Enock Mwesiga.