December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yavuna tril 1.8 kupitia sekta ya uziduaji nchini

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

SERIKALI imepata jumla ya shilingi Trilion 1.877 kutoka kwenye kampuni 44 zilizolinganishwa katika sekta ya madini, mafuta na gesi ikiwa na tofauti ya kati ya malipo na mapato ya shilingi milioni 402.41 kwa mwaka kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa wa Madini Anthony Mavunde katika uzinduzi wa ripoti ya 14 ya Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji Katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) uliofanyika jijini Dar es Salaam. Mavunde amesema kati ya kampuni hizo, kampuni 26 ni za Madini; Kampuni saba ni za gesi asilia na mafuta; na Kampuni 11 ni kampuni zinazotoa huduma katika sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia.

Amesema, kampuni zilionesha kuwa zililipa kiasi cha shilingi trillion 1.878serikalini na kupelekea kuwepo na tofauti kati ya malipo na mapato ya shilingi milioni 402 sawa na asilimia asilimia 0.021 ya mapato yote yaliyoripotiwa na Serikali.

Aidha, Mavunde ameelekeza, tofauti hiyo sh milioni 402 kufanyiwa uchambuzi wa kina ili kujua visababishi vilivyosababisha kutofautiana ili Kamati iweze kuzipa makampuni na serikaliushauri wa nini kifanyike ili tofauti hizo zisiendelee kujitokeza kwenye linganishi zitakazofuata.

Amesema, pamoja na masuala mengine yaliyomo ripoti hiyo ya TEITI pia imeweka wazi taarifa mbalimbali ili kutekeleza matakwa ya Viwango vya Kimataifa vya EITI pamoja na Sheria inayosimamia shughuli za TEITI nchini.

Mavunde amesema, taarifa hizo ni pamoja na takwimu za uzalishaji na usafirishaji wa rasilimali madini, mafuta na gesi asilia (Production and export data), takwimu za ajira katika sekta ya uziduaji, michango ya kampuni kwa jamii (Corporate Social Responsibilities-CSR) na ushiriki wa wazawa katika sekta ya uziduaji ikijumuisha kutoa huduma kwenye kampuni za uziduaji (Local content).

Awali, akizungumza katika hafla hiyo,Mwenyekiti wa kamati ya TEITI, Ludovick Utouh amesema lengo la uzinduzi wa ripoti hiyo ni kuweka wazi kwa ajili ya wananchi na wadau mbalimbali ili waweze kutumia takwimu zilizomo kufanya mijadala ya kuboresha na kuongeza mchango wa sekta ya madini, mafuta na gesi asilia katika Pato la Taifa.

Nae, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dkt. David Mathayo ameipongeza serikali kwa kutoa taarifa ya wazi ya ulinganisho wa mapato yatokanayo na sekta ya uziduaji na kutumia fursa hiyo kuwataka watanzania waipitie na kuona namna ambavyo sekta hii ya uziduaji inavyochangia kukuza uchumi wa nchi na kuwataka pia wananchi kutumia taarifa hii kushauri na kutoa maoni yao.