Na Joyce Kasiki,TimesMajira Online,Dodoma
SERIKALI imetoa muda wa miezi mitatu kwa ajili ya vifungashio vya visivyokidhi Viwango vya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuondolewa sokoni.
Agizo hilo la Serikali limetolewa juzi jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu.
Amesema licha ya Serikali kupiga matumizi ya mifuko ya plastiki, lakini siku za hivi karibuni kumejitokeza changamoto yq matumizi ya vifungashio vya plastiki aina ya ‘tubings’ visivyokuwa na sifa na hivyo kutokidhi matakwa yaliyowekwa na TBS.
Amesema vifungashio hivyo kwa sasa vinazalishwa kwa wingi na kwa ukubwa mbalimbali na vimekuwa vikitumika kama mifuko ya kubebea bidhaa sokoni na kuleta dhana kuwa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku imerudi kivingine.
“Mifuko hiyo imeanza kuzagaa kwenye mazingira ya mitaa yetu na vijijini vyetu kwa kasi kubwa na hivyo kurudisha nyuma mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kipindi chote cha kupambana na changamoto ya mifuko hiyo.” amesema Waziri Ummy na kuongeza;
“Vifungashio vinapaswa viwe na unene usiopungua microns 30 upande mmoja au microns 60 pande mbili, kilichofungashiwa bidhaa ili kukuza kabla ya kwenda sokoni viwe na alama ya mzalishaji au anayepakia bidhaa, lakini pia viwe na alama ya ubora inayotolewa na TBS.”
Ummy amewataka wasambazaji wazalishaji wa vifungashio hivi na waagizaji kuacha mara moja kuzalisha, kusambaza kuuza na kutumia vifungashio hivyo.
Ametoa muda huo wa miezi mitatu vifungashio hivyo kuondoka sokoni vifungashio hivyo kutokana na wafanyabiashara wadogo kuonekana bado wana shehena ya vifungashio hivyo.
“Kwa kuzingatia maombi ya wafanyabiashara wadogo ambao bado wana shehena ya vifungashio hivi na kwa kuwa Serikali ya awamu ya tano inathamini mchango wa wafanyabiashara wadogo katika juhudi za kujiongezea kipato katika kupambana na umasikini natoa kipindi cha miezi mitatu kuanzia siku ya tangazo hili kuhakikisha kwamba vifungashio visivyokidhi viwango vya TBS havipo sokoni,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Waziri Ummy baada ya kipindi hicho Serikali haitatoa tangazo jingine lolote kuhusiana na katazo la matumizi ya vifungashio hivyo na badala yake itaendesha operesheni maalum kuwabaini wanaozalisha na kuvisambaza na kuwachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwatoa hofu wananchi kwamba hakutakuwa na uhaba wa vifungashio vinavyokidhi viwango baada ya kipindi hicho cha miezi mitatu kwa kuwa kwa mujibu wa TBS wapo wazalishaji wa kutosha wa vifungashio hivyo kukidhi mahitaji yaliyopo nchini.
Amewaasa wazalishaji na wawekezaji wa ndani kuchangamkia fursa hiyo kwa kuzalisha vifungashio vyenye ubora unaotakiwa.
Juni Mosi, 2019 Serikali ilipiga marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki nchini ambapo tangazo hilo lilihusu kuzuia uzalishaji, uingizaji nchini, uuzaji ,uhifadhi ,usambazaji ,matumizi ya mifuko ya plastiki nchini na umiliki wa mifuko hiyo kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyo.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua