Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa wamewapeleka Kamishina wa Elimu,Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora pamoja na Mwanasheria wa Wizara kufatilia taarifa inayohusu shule ambazo zinafundisha wanafunzi kulawitiana.
Amesema kuwa Taarifa hiyo iliripotiwa hivi karibuni na chombo cha habari ambapo imeelezwa kuwa tukio hilo la wanafunzi kulawitiana limetokea Moshi mkoa wa Kilimanjaro
Prof.Mkenda amesema hayo jijini hapa leo,Januari,17,2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kwa sasa timu hiyo wanapitia hizo shule na kupata taarifa lakini pia wamemuomba mkuu wa mkoa kushirikiana natimu hiyo ,pamoja na kuwasaidia sehemu ambayo inamasuala ya jinai polisi wachukue hatua.
“Tunatarajia kwamba hao walioenda wataleta taarifa kamili na sisi tukotayari kuchukua hatua stahiki kudhibiti mambo hayo, zaidi ya hayo kwakuwa suala hili limetokea eneo moja basi tunajua kunaweza kukawa na taarifa kwenye maeneo mengine hivyo sisi kama wizara katibu mkuu atatoa namba ambayo mtu yeyote ambaye akijua kuna kitu kama hicho katika shule yeyote iwe ya umma au binafsi au vyuo vyovyote hapa nchini anaweza akapiga simu akatupa taarifa,
“Tutafatilia kwa nchi nzima tunaongeza umakini kwa kufatilia mambo haya kwasababu tunajua yanaweza kuchafua taswira ya elimu,yanaharibu vijana wetu na hata wazazi kukosa imani na shule ,na katibu mkuu leo atatangaza namba”amesema Prof.Mkenda.
Pamoja na hayo Prof.Mkenda amesema pia walifanya mkutano ambao ulikuwa chini ya Mwenyekiti Simbachawene,Waziri wa Maendeleo ya jamii,Dkt.Doroth Gwajima na Waziri wa Utumishi Angela Kairuki pamoja na makatibu wakuu kwaajili ya kuangalia namna ya kudhibiti mambo hayo.
“Tumeanza mkakati wa kitaifa wa kuangalia namna ya kudhibiti mambo hayo ambayo yanatokea Mashuleni,Majumbani, Njiani na maeneo mbalimbali hivyo kwahiyo siyo swala la wizara moja ni swala mtambuka kwahiyo kazi inaendea na Makatibu wakuu watarudisha taarifa yao halafu tutakuwa na mkakati mzuri zaidi kitaifa,”amesema.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best