April 3, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatoa fursa kwa wahitimu kidato Cha nne 2024 kubadilisha Tahasusi

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa,amewataka wahitimu wa kidato Cha nne  kwa mwaka 2024 ,kufanya mabadiliko ya tahasusi (combination) kulingana na ufaulu wao utakaowawezesha kuoangiwa kidato Cha Tano na vyuo kwa mwaka 2025.

Amesema zoezi hilo la kubadili tahasusi limeanza Machi 31 na litafunhwa  April 31 mwaka huu .

Mchengerwa ameyasema hayo Leo April 2,2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa kwa wahitimu wa kidato Cha mwaka 2024 kufanya mabadiliko ya tahasusi za kidato Cha Tano na kozi za vyuo kwa njia ya mtandao kwenye mfumo wa Uchaguzi wa wanafunzi wa kidato Cha Tano na vyuo mwaka 2025.

“Leo nimewaita hapa kwa ajili ya kutoa taarifa muhimu kwa wahitimu wa Kidato cha Nne mwaka 2024 kuhusu fursa ya kubadilisha machaguo ya Tahasusi za Kidato cha Tano na Vyuo vya Kati na Elimu ya Ufundi kwenye mfumo wa kielektroniki wa uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na Kidato cha Tano na Vyuo.”amesema Mchengerwa

Amesema hayo ni  maandalizi ya awali ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga Kidato cha Tano na Vyuo vya Serikali Mwaka, 2025. 

Waziri Mchengerwa amesema, Serikali imekuwa ikitoa fursa kwa wahitimu wa Kidato cha Nne kufanya mabadiliko ya machaguo ya Tahasusi (combination) na Kozi mbalimbali walizozichagua kupitia Fomu ya Uchaguzi .

Amesema,fursa hiyo huwawezesha wanafunzi kurekebisha machaguo yao kulingana na ufaulu waliopata kwenye matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA).

Aidha amesema,Serikali kupitia Ofisi ya Rais  TAMISEMI imekamilisha zoezi la awali la kuingiza kwenye kanzidata taarifa zilizo kwenye Fomu za Uchaguzi za wanafunzi kama zilivyojazwa na wanafunzi wakiwa shuleni. 

“Kukamilika kwa zoezi hili kunatoa fursa kwa wanafunzi kuweza kufanya mabadiliko ya machaguo/ tahasusi/ kozi kwa njia ya mtandao ambapo baada ya wanafunzi kufanya marekebisho yao, kanzidata hiyo ndiyo itakayotumika kuwachagua na kuwapangia nafasi za Kidato cha Tano na Kozi mbalimbali katika Vyuo vya Kati na vya Elimu ya Ufundi kwa kuzingatia sifa za ufaulu na machaguo yao. “Amesema Mchengerwa

Amesema,Ofisi ya Rais  TAMISEMI inatoa fursa kwa wahitimu wa elimu ya sekondari Kidato cha Nne, mwaka 2024 kubadili machaguo yao ili kutoa nafasi zaidi kwa mwanafunzi kusoma tahasusi au kozi itakayomwandaa kuwa na utaalamu stahiki katika maisha yake ya baadaye. 

Kwa.mujibu wa Mchengerwa,zoezi hilo litatoa fursa zaidi ya wanafunzi kuongeza machaguo na kufanya machaguo mapya ya Tahasusi na Kozi.

Amewaasa   wazazi/ walezi kushiriki katika zoezi hili kwa kushauriana na watoto wao katika kufanya machaguo sahihi kulingana na ufaulu wao lakini pia,amewahimiza  wahitimu wote  kufanya marekebisho ya machaguo ya tahasusi na kozi kulingana na ufaulu wao, kwa kuingia kwenye Mfumo wa Uchaguzi wa Wanafunzi unaopatikana kupitia kiunganishi cha selform.tamisemi.go.tz

Aidha amesema,maelekezo kwa wahitimu na jinsi ya kufanya mabadiliko watayapata kwenye mfumo kupitia ‘user manual’ pamoja na video ya youtube zilizopo kwenye mfumo huo.

Amesema,ili kuingia kwenye mfumo  mhitimu anapasqa atumie Namba yake ya  Mtihani wa kuhitimu Kidato cha Nne mwaka 2024, Jina lake la Mwisho, Mwaka wa Kuzaliwa na Alama ya Ufaulu aliyopata kwenye somo atakaloulizwa na mfumo au swali lolote atakaloulizwa.

“Ni matumaini yangu kuwa wahitimu wote watatumia kwa ukamilifu fursa waliyopewa ya kubadilisha Tahasusi na Kozi kulingana na ufaulu waliopata na pia wataweza kusoma tahasusi/kozi ambazo wamefaulu vizuri ama wana malengo nazo zaidi. “

Waziri huyo amewasisitiza wasisitiza wanafunzi, wazazi/ walezi kutumia muda huo vyema ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza mara baada ya matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo kutangazwa huku akisema ni muhimu kuzingatia muda uliotolewa wa kufanya marekebisho ili ratiba ya kuwachagua na kuwapangia shule na vyuo iweze kuendelea kwa muda uliopangwa. 

Aidha amesema huduma hiyo ya kubadilisha tahasusi ni bure na endapo wanafunzi watapata changamoto, wawasiliane na Dawati la Huduma la Mteja kupitia barua pepe: huduma@tamisemi.go.tz au kuwasiliana moja kwa moja na Kituo cha Huduma kwa Wateja kwa simu +255 262 160 210 na +255 735 160 210. 

Aidha amesema, pamoja na maelekezo hayo, kwa mwanafunzi, mzazi/mlezi atakayekuwa na suala linalohitaji maelezo au ufafanuzi zaidi aende katika Ofisi za Elimu za Mikoa na Halmashauri.