December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatoa eneo la kujenga bandari Kilwa

Na Mwandishi wetu,timesmajira.

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inakusudia kutenga eneo lenye ukubwa wa hekari 1. 644 kutoka katika msitu wa hifadhi ya Mikoko Kilwa Masoko mkoani Lindi kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, Jijini Dodoma wakati wa kikao kazi na Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Deusdedith Bwoyo na Wataalam wa Sheria wa Wizara hiyo akieleza kuwa kutolewa kwa eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa bandari ni moja ya mikakati ya Serikali ya kuboresha sekta ya Utalii ili kwenda na matokeo chanya ya Filamu ya The Royal Tour.

Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana ameendeleaa kumshukuru Rais wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada mbalimbali anazozifanya kuinua sekta ya Maliasili na Utalii hasa kupitia programu ya The Tanzania Royal Tour ambayo imevutia watalii wengi kuingia nchini.

Aidha, amesema Wizara anayoingoza inaendela kupanua wigo wa mazao mapya ya Utalii hivyo kuwepo kwa Bandari ya Uvuvi katika eneo la hifadhi wilayani Kilwa kutasaidia kuchochea Utalii wa Uvuvi jambo ambalo litavutia watalii wengi hasa wenye kupenda masuala ya uvuvi.

Balozi Dkt. Pindi Chana ameongeza kuwa ujenzi wa bandari hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/2025 ambayo imeainisha masuala mbalimbali yanayopaswa kutekelezwa yakiwemo ya kuongeza ajira, kuongeza mapato kwa wananchi na Serikali pamoja na idadi ya watalii hapa nchini.

Katika kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa na uhifadhi endelevu Waziri Balozi Dkt. Chana ametoa rai kwa wananchi waendelee kushirikiana na Serikali katika kutunza Hifadhi za Taifa hususani maeneo ya misitu ili wazuie changamoto ya moto, vitendo vya kuingiza mifugo na kuanzisha shughuli mbalimbali za kijamii ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa.

Amesema kwa sasa Tanzania inapata watalii wengi kutokana na kazi nzuri ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Program ya The Royal Tour, huku akitoa rai kwa wananchi kutunza hifadhi za Misitu.