January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatoa bilioni 3.46 kukarabati Vyuo vya ufundi stadi na watu wenye ulemavu

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

SERIKALI imetoa kiasi cha shilingi bilioni 3.46 kwajili ya ukarabati vyuo vya Ufundi Stadi na marekebisho kwa watu wenye ulemavu nchini.

Hayo yameelezwa Jijini hapa leo,Disemba 14,2023 na Naibu Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na wenye Ulemavu,Patrobas Katambi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu baadhi ya shughuli zilizotekelezwa na zinazoendelea kutekelezwa na Wizara hiyo.

Katambi ametaja maeneo vilivyopo vyuo hivyo vinavvyotakiwa kukarabatiwa kuwa ni Sabasaba-Singida,Yombo-Dar es Salaam,Mtapika-Masasi na Luanzari-Tabora.

Aidha amesema kuwa Serikali imeendelea kutoa mafunzo kuputia vyuo sita vya Ufundi stadi na Marekebisho kwa watu wenye Ulemavu na vijana wenye ulemavu wapatao 774 na kiasi cha shilingi milioni 568 kimetumika kuwezesha mafunzo hayo.

Akizungumzia maendeleo mengine Katambi amesema serikali imejipanga kutengeneza mfumo wa kitaifa wa Kieletroniki wa taarifa za soko la ajira wenye gharama ya shilingi 346,920,000 kwajili ya kuwezesha ukusanyaji wa taarifa kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Taifa.

Katambi amesema kuwa kutengenezwa kwa mfumo huo kutaondoa wananchi kutapeliwa kutokana na taarifa feki zinazotumwa kwenye mitandao zikipotosha kuhusu kuwepo kwa ajira katika taasisi mbalimbali za serikali.

“Mfumo huu ukikamilika utakomesha matapeli wanaotuma taarifa feki kuhusu kuwepo kwa ajira feki ambazo huleta taharuki kwa wananchi,”amesema Katambi.

Vilevile amesema Serikali imetoa kiasi cha Shilingi bilioni 4.26 kwajili ya ununuzi wa vifaa vya usikivu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na vifaa husika vimeshanunuliwa na kusambazwa katika shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum.

“Serikali imeendelea kusimamia maadhimisho ya kimataifa ya watu wenye ulemavu nchini yakiwemo maadhimisho ya siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu,wiki ya viziwa,siku ya kimataifa ya fimbo nyeupe na siku ya watu wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi.

“Lengo kuu la maadhimisho haya ni kuongeza uelewa wa haki na ustawi wa watu wenye ulemavu katika jamii kutambua shughuli na vipaji vya watu wenye ulemavu na kuimarisha umoja na mshikamano.