November 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatishia kuwasimamishia mishara Maofisa Utumishi

Na James Mwanamyoto,TimesMajira Online. Dodoma

MAOFISA Utumishi watakaozembea na kusababisha watumishi wa umma kutolipwa mishahara yao kwa wakati, watasimamishiwa mishahara na serikali mpaka watakapohakikisha watumishi hao wamelipwa mishahara yao.

Hayo yamesemwa jana na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael wakati akifungua mafunzo ya wiki mbili ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara kwa kundi la pili la Maofisa Utumishi na Maofisa Tawala 140 kutoka Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Kigoma na Tabora yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.

DKt. Michael amesema, kuna tatizo katika baadhi ya taasisi za umma kwani wapo Maofisa Utumishi wanajifanya miungu watu, wakati wajibu wao ni kumtengenezea mazingira mazuri ya kikazi mtumishi ili ajisikie yuko sehemu salama na aweze kutekeleza ipasavyo jukumu la kuwahudumia wananchi.

“Msiwafanye watumishi mnaowasimamia kuona sehemu ya kazi kama jehanamu, hivyo mbadilike kwani serikali haitomvumilia yeyote atakayekinzana na azma yake ya kuboresha huduma kwa wananchi,” amesema.