Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu, amewataka waajiri wote katika Sekta ya Umma kutekeleza kwa wakati mwongozo wa upandishaji vyeo na ubadilishaji kada kwa watumishi waliocheleweshwa kupandishwa vyeo.
Akijibu swali la msingi kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalum, Dkt. Alice Kaijage, Naibu Waziri Sangu amesema utekelezaji wa hatua hiyo utasaidia kuondoa malalamiko kutoka kwa watumishi wa umma wanaokumbwa na changamoto ya kucheleweshewa madaraja.
Katika swali lake, Dkt. Kaijage alitaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuhakikisha kuwa kada nyingine katika utumishi wa umma zinapewa madaraja ya mserereko kama ilivyo kwa Kada ya Ualimu.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 6(1)(b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298, jukumu la kuwapandisha vyeo watumishi wa umma ni la mwajiri husika. Jukumu hilo hutekelezwa baada ya Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kutoa mwongozo kwa waajiri kuandaa na kuwasilisha Ikama na Bajeti ya mwaka husika, na baada ya bajeti hiyo kuridhiwa.
Naibu Waziri Sangu alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali iliwapandisha vyeo kwa mserereko watumishi 1,284 wasiokuwa walimu. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali tayari imetoa mwongozo unaohusu upandishaji vyeo na ubadilishaji wa kada, ikiwa ni pamoja na kwa watumishi waliocheleweshwa kupandishwa vyeo.
Katika swali la nyongeza, Dkt. Kaijage alitaka kufahamu mkakati wa Serikali wa kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miongozo ya upandishaji madaraja na ubadilishaji wa kada, ili kuhakikisha kuwa hatua hizo zinachukuliwa kwa wakati na kupunguza malalamiko ya watumishi.
Akijibu, Naibu Waziri Sangu alisisitiza kuwa waajiri wote ambao bado hawajapeleka majina ya watumishi wanaostahili kupandishwa vyeo na kubadilishiwa kada wanapaswa kufanya hivyo mara moja, kwani tarehe ya mwisho ilikuwa mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu.
“Nikuhakikishie kuwa jambo hili tutalifuatilia kwa karibu. Waajiri wengi tayari wameitikia na kutekeleza suala hili, lakini natumia fursa hii kutoa rai kwa wale ambao bado hawajakamilisha, kuhakikisha ndani ya wiki moja wanawasilisha taarifa hizo. Lengo letu ni kuhakikisha tunapoanza mwaka mpya wa fedha, watumishi wote wawe wamepandishwa vyeo kwa mujibu wa bajeti ya takribani shilingi bilioni 207,” alisema Sangu.
Aidha, alibainisha kuwa kasi ya utekelezaji wa upandishaji vyeo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo bajeti ipo na dhamira ni kuhakikisha ifikapo mwaka mpya wa fedha 2025/2026, kusiwepo malalamiko yoyote ya watumishi waliolimbikizwa madaraja.
Aijibu swali hilo,Naibu Waziri Sangu amewataka waajiri wote ambao Bado hawajapeleka majina ya watumishi wa Umma wanapaswa kupandishwa vyeo na kubadilishiwa kada,wafanye hivyo mara Moja kwani mwishonwa kupeleka ilikuwa ni mwishoni mwa mwezi Mei

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi