Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
SERIKALI imetenga kiasi cha shilingi bilioni 6.4 mwaka wa fedha 2022/23 kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation-HEET) kwa ajili ya kuimarisha uthibiti ubora na uhuishaji wa mitaala ya vyuo vikuu nchini.
Hayo yamsemwa jijini hapa leo,Februari 22,2023 na Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania(TCU), Prof.Charles Kihampa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo.
Prof.Kihampa amesema kuwa kupitia mradi huo zaidi ya mitaala 300 ya vyuo vikuu iko katika hatua mbalimbali za kufanyiwa mapitio ili kuhuishwa kwa kuzingatia maoni ya wadau mbalimbali ili kukidhi matarajio yao na mahitaji ya soko.
“Katika kufanikisha hili, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, imeendelea kuandaa na kuratibu mafunzo ya kubadilishana uzoefu kwa viongozi na wanataaluma wa vyuo vikuu kuhusiana na uendeshaji wa vyuo vikuu, utengenezaji mitaala inayozingatia ujuzi na inayoendana na soko, mbinu za ufundishaji kwa wahadhiri ambao hawakusoma fani za ualimu, ulinganifu wa programu za masomo (programme benchmarks), uthibiti ubora, na utengenezaji na utumiaji wa mifumo ya kompyuta,
“Kwa mfano, katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2022 jumla ya viongozi na wanataaluma 575 wameshanufaika na mafunzo hayo na Mafunzo hayo yamelipiwa na serikali kwa asilimia 100,”amesema.
Prof.Kihampa amesema kutokana na hatua hizi zinazochukuliwa na Serikali, vyuo vikuu vimeweza kuimarisha mifumo yake ya uthibithi ubora na uendeshaji wa mafunzo pamoja na kuongezeka kwa fursa za masomo ya elimu ya juu na idadi ya wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya elimu ya juu nchini.
Akizungumzia mafanikio ya Tume hiyo Prof.Kihampa amesema kuwa mifumo ya uthibiti ubora, ushauri na usimamizi wa elimu inayotolewa na Vyuo Vikuu hapa nchini imeimarika.
“Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania imeendelea kuimarisha mifumo yake ya uthibiti ubora na mifumo ya ndani ya vyuo vikuu ili kuhakikisha vyuo vikuu vinaendana na mwelekeo wa nchi, ambapo Tanzania imelenga kuwa Taifa la watu wenye maarifa, ujuzi, weledi na uwezo wa kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wake ifikapo mwaka 2025 pamoja na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaochochewa na uwepo wa viwanda,”amesema.
Pia amesema katika kuhakiki ubora, TCU imeimarisha mifumo yake ya ushauri na ukaguzi wa mara kwa mara, wa kawaida na wa kushtukiza kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo kwa lengo la kuhakikisha kuwa elimu itolewayo na vyuo vikuu hapa nchini inakidhi viwango vya ubora kitaifa, kikanda, na kimataifa. Kwa mfano, katika kipindi cha Julai 2021 hadi Februari, 2023 vyuo vikuu vyote 47 vilivyopo vimekaguliwa na kupewa ushauri wa maeneo yanayohitaji kuboreshwa.
“Zoezi hili la ukaguzi wa vyuo ni endelevu kila mwaka. Vilevile TCU imeweka utaratibu wa kuanzishwa na kuimarishwa mifumo ya uthibiti ubora ndani ya vyuo vikuu ambapo vyuo vyenyewe vimekua na utaratibu wa kujikagua, kujitathmini na kufanya marekebisho mbalimbali kwa kuzingatia miongozo ya uendeshaji wa vyuo vikuu,”amesema.
Ameeleza kuwa mifumo ya ushauri, ukaguzi, na ufuatiliaji wa mara kwa mara imefanya vyuo kufanya maboresho makubwa katika miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maabara za kisasa, mifumo ya mawasiliano ya kielektroniki, madarasa na kuongeza idadi ya viongozi na wahadhiri wenye sifa stahiki kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo iliyopo.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best