Na Happiness Shayo,TimesMajira Online,Dodoma
SERIKALIi kupitia Wizara ya Maji imeipatia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) kiasi cha shilingi bilioni 1 ili kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo yenye changamoto ya huduma hiyo jijini Dodoma.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga alipotembelea kisima kimojawapo kati ya visima vinavyochimbwa katika eneo la Ihumwa jijini Dodoma.
“Hili linafanyika kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma ya maji katika maeneo mbalimbaji ya jiji la Dodoma hasa maeneo ya pembezoni” amesema Mhandisi Sanga.
Aidha,amefafanua kuwa kuhamia kwa Serikali jijini Dodoma ni fursa kwa taasisi za maji zilizoko Dodoma kutatua changamoto za huduma ya maji wanazozipata wananchi wa Dodoma.
Mhandisi Sanga amongeza kuwa Serikali ina mipango ya muda mfupi, ya kati na ya muda mrefu ya kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma ya maji.
“Mipango ya muda mfupi ni kama ujenzi wa visima vya dharula katika eneo la Ihumwa na mipango ya muda wa kati ni ujenzi wa bwawa la Farkwa na muda mrefu ni kutoa maji kutoka ziwa Victoria” amefafanua Mhandisi Sanga.
Naye,Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi David Pallangyo ameongeza kuwa ujenzi wa kisima hicho eneo la Ihumwa ni mojawapo ya visima kadhaa vitakavyoweza kuzalisha maji na kuyatoa kuyapeleka hadi mjini ili kupunguza tatizo la maji eneo la mjini.
“Vitachimbwa visima vinavyozalisha si chini ya mita za ujazo elfu tatu kwa siku zitakazosaidia kupunguza tatizo la maji maeneo ya pembezoni kama Mwangaza, Njedengwa, Ihumwa na maeneo mengine ya mjini.
Mhandisi Pallyangyo amesema mradi wa ujenzi wa visima eneo la Ihumwa utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.4.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge ameupongeza uongozi wa DUWASA kwa kutatua changamoto za maji jijini Dodoma na kuwataka kuongeza ushirikiano ili kufikia malengo.
Lengo la juhudi zote za Serikali ni kuhakikisha huduma ya majisafi na uondoshaji wa majitaka zinakuwa za uhakika zinazoendana na hadhi ya jiji la Dodoma ambalo ndio makuu ya nchi.
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani