Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online
Tanzania inajivunia kutekeleza kwa vitendo hatua za kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki katika ngazi zote za elimu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda amesema hayo Oktoba 11, 2023 jijini Dodoma katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike yaliyojikita kusherehekea mafanikio ya mtoto wa kike kwenye elimu na kufanyika jijini Dodoma
Ametaja baadhi ya mafanikio ambayo Tanzania inajivunia kwenye elimu kuwa ni pamoja na mpango wa kuwarejesha shule wanafunzi waliokatisha masomo wakiwemo wasichana.
Ameongeza kuwa kupitia mpango huo wanafunzi wa kike 7,995 wamerejea shule kupitia mfumo rasmi na usio rasmi kupata elimu ili kutimiza ndoto zao.
Prof. Mkenda amesema juhudi mbalimbali zilizofanyika Tanzania ni pamoja na kupitia Sera, Sheria na Nyaraka mbalimbali ili kuhakikisha watoto wote akiwemo wa kike anapata fursa sawa ya elimu. Ametaja baadhi ya juhudi hizo kuwa ni kutungwa kwa sheria ya Haki za Mtoto ya mwaka 2009 na kutoa Waraka wa Elimu Na. 3 wa mwaka 2021 kuhusu urejeshwaji wa wanafunzi waliokatisha masomo katika elimu ya sekondari na msingi.
“Nina salamu zangu kwa UNICEF naialika ishirikiane na wizara yetu ya elimu kufanya utafiti kwa kufuatilia wale wote ambao wamerudi shule mmoja mmoja kumhoji kuangalia mazingira, mafanikio, changamoto na kuja na mapendekezo ya namna bora zaidi ya kutekeleza maelekezo haya ya Rais Samia ya kuhakikisha hakuna mtoto atakayeachwa nyuma kwenye elimu,”amesema Prof. Mkenda.
Aidha, amesema wanafunzi wa kike wananufaika na mikopo na kwa Mwaka 2022/23 serikali ilianza mpango wa Samia Scholarship kwa wanafunzi waliofaulu vizuri kwenye masomo ya sayansi kidato. Kati ya wanfunzi 636 walionufaikawanafunzi wa kike 261 sawa na asilimia 41.
“Kumekuwapo na mazingira wezeshi kupitia miongozo, miundombinu na vifaa mbalimbali yaliwezesha watoto wenye mahitaji maalum kupata elimu, kila mwaka serikali inatenga fedha ya kununua vifaa,”amesema Prof Mkenda.
Waziri Mkenda pia amesema idadi ya wanafunzi waliodahiliwa katika Taasisi za Elimu ya Juu imeongezeka kwa asilimia 31 kutoka wanafunzi 423,025 ambapo kati yao wa kike ni 177,905 kwa mwaka 2019/20 hadi kufikia wanafunzi 555,166 ambapo kati yao wa kike ni 249,009 kwa mwaka 2022/23.
Akizungumzia walionufaika na mikopo ya elimu ya juu, amesema idadi yao imeongezeka kutoka wanafunzi 131,659 kwa mwaka 2019/20 hadi kufikia wanafunzi 202,016 kwa mwaka 2022/23 na ongezeko hili ni sawa na ongezeko la asilimia 53, miongoni mwa wanufaika ni wanafunzi wa kike ambao idafi yao pia imeongezeka kutoka 50,145 kwa mwaka 2019/20 kufikia 85,793 kwa mwaka 2022/23 ongezeko hili ni sawa na asilimia 71.
“Wizara imejenga shule mpya 26 za wasichana za mchepuo wa Sayansi ambapo kila mkoa Tanzania bara umejengewa shule moja lakini pia na shule nyingine moja inajengwa wa kila kata.
” shule hizi zote zitanufaisha watoto wa kike na wakiume na pia kusaidia kupunguza umbali kutoka nyumbani kwenda shuleni jambo ambalo limepunguza changamoto ambazo wangekutana nazo wakati wa kwenda shule hasa wanafunzi wa kike,”amesema Prof. Mkenda.
Ametewataka wanafunzi wa kike kote ncjini wakiwemo waliorejea Shule kujikita na kuxongatia masomo ili kufikia ndoto zao. Huku akisiditiza kuwa Wizara itaendelea kuimarisha miundombinu na mazingira ya utoaji elimu bora kwa usawa kwa watoto wote ikiwemo wenye mahitaji maalum bila.
Mkenda ameishukuri UNICEF kwa kuungana na Wizara kuadhimisha mafanikio haya katika siku muhimu ya kimataifa ya Mtoto wa kike.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe. Husna Sekiboko, amesema Bunge na kamati haitakuwa kikwazo katika mipango ya serikali ya kumuendeleza na kumlinda mtoto wa kike nchini.
“Tutahakikisha watoto wa kike wanatimiza ndoto zao na si jambo la kufikiria wewe Mheshimiwa waziri ni shahidi wabunge walichangishana na kujenga shule ya wasichana ya Bunge kwa lengo la kuionesha serikali na jamii kwamba wabunge wanaunga jitihada za kumlea na kumlinda mtoto wa kike Tanzania,”amesema Prof Mkenda.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini, Dkt.Daniel Baheta, amesema shirika hilo litaendelea kujitolea kuunga mkono jitihada za serikali katika kuwaendeleza wasichana na kuwawezesha.
“Tumeshuhudia serikali ikiondoa vikwazo vinavyokwamisha upatikanaji wa elimu bora kwa wasichana na uamuzi wa kuruhusu wasichana wajawazito, watu wazima na wasichana, mama vijana kurudi shule tunapongeza sana,”amesema Dkt Baheta.
Mmoja wa wanufaika wa Mradi wa SEQUIP qmbae amerejea shule, Neema Chaopa, amemshukuru Rais Samia kwa kuwafuta machozi watoto wa kike kupitia mradi huo ambao wengi wao walikuwa wamekata tamaa baada ya kukatisha masomo yao kwa sababu mbalimbali.
“Kupitia mradi wa SEQUIP tumefutwa machozi tumerejesha ndoto zetu upya wengine tulitamani kuwa waandishi wa habari. Watoto wa kike tumepewa fursa nyingine yakurudisha ndoto zetu.”
Na kuongeza “Tunasoma na wengine kutoka mikoa mbalimbali kupitia Taasisi ya Watu Wazima, kuna mabinti waliokatisha kwa ujauzito walikuwa wanauza mboga, wengine walishakuwa wafanyakazi wa ndani katika umri mdogo lakini kwa tamko la mama sisi tukarudi shuleni, leo tena tumesimama, tumependeza,”
Awali, Mkurugenzi wa Elimu kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Susan Nussu, amesema Ofisi hiyo imesimama imara kusimamia viongozi wote kuanzia ngazi za chini kuhakikisha watoto wa kike wanakuwa kwenye mazingira salama.
More Stories
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi
Muhoji Sekondari kumaliza changamoto ya umbali kwa wanafunzi Musoma vijijini
Tanzania mwenyeji mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika