Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC) itasambaza na kuunganisha bila malipo miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia kwa matumizi ya majumbani kwa wateja wa awali katika mikoa yote itayofikiwa na huduma hiyo nchini.
Hayo ameyabainisha wakati akizindua mradi wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia kwa matumizi ya majumbani katika Kijiji cha Mnazi Mmoja mkoani Lindi.
Pia Waziri amewataka wakazi wa eneo hilo kuchangamkia fursa hiyo ili kujiletea maendeleo na kuondokana na uchafuzi wa mazingira, gharama kubwa za kununua mkaa na kuni pamoja na adha kutafuta kuni porini kwa ajili ya kupikia, kwani matumizi ya gesi ni salama na nafuu.
Amesema kuwa, baada ya wateja hao kuunganishiwa miundombinu ya kusambaza gesi asilia katika nyumba zao zikiwemo taasisi mbalimbali, mteja atawekewa mita ya kupimia kiasi cha gesi anayotumia itakayofanya kazi kama LUKU za umeme nchini.
Alisema baada ya kufungiwa miundombinu hiyo ya kusambaza gesi asilia, mteja atatakiwa kununua uniti za gesi kulingana na mahitaji yake kama ilivyo katika umeme, na kuzitumia endapo zitaisha kabla ya kuongeza nyingine, mita itafunga hadi pale atakaponunua uniti zingine kuongezea, mfumo huo unaitwa malipo kabla ya kutumia( Pre- Paid System).
Waziri amesema, kwa familia ya watu sita inakadiriwa kutumia kiasi cha gesi ya shilingi 30,000 tu, kwa mwezi kwa matumizi yote ya kupikia bila kubagua aina ya vyakula vinavyotumia muda mrefu jikoni.
Waziri Dkt.Kalemani amesema, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John Magufuli imeamua kufanya hivyo ili kuhamasisha matumizi ya gesi asilia iliyopatikana kwa wingi hapa nchini.
Sambamba na kupunguza ukataji wa miti ovyo kwa ajili ya kuni na kuchoma mkaa ili kusaidia juhudi za kutunza na kuhifadhi mazingira yetu, hatua ambayo itawezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Pia amesema,mradi wa usambazaji wa gesi asilia ni endelevu, ambapo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 wateja wapya 2,000 wataunganishia gesi majumbani, 300 kati yao wanatoka Mkoa wa Lindi na vitongoji vyake.
Alitaja mikoa inayofuata sasa katika utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kusambaza gesi asilia kuwa ni pamoja na Morogoro, Dodoma na Singida.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC , Dkt. James Mtaragio amewatoa hofu watumiaji wa gesi asilia majumbani kwa kuwaeleza kuwa, usanifu na ujenzi wa miundombinu hiyo imezingatia hatua zote za usalama.
Amesema, lengo la kufanya hivyo ni ili kuhakikisha matumizi ya gesi hiyo yanakuwa salama zaidi kwa mtumiaji na jamii kwa ujumla.
Dkt.Mataragio pia amewaomba wananchi kuondoa hofu katika matumizi ya gesi asilia kwa shughuli za kupikia.
Dkt.Matargio akizungumzia gharama za matumizi ya gesi hiyo ikilinganishwa na mkaa pamoja na kuni amesema kuwa, kwa ulinganishi matumizi ya mkaa si chini ya shilingi 4,500 kwa,wakati matumizi hayo hayo kwa kutumia gesi ni shilingi 1000 tu kwa kupikia.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amesema kuwa, Mkoa wa Lindi umeandika historia nyingine iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu ya ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia itakayokuwa ikitumika kwa kupikia majumbani, mahotelini kwenye taasisi za afya, elimu na matumizi mengineyo kama viwandani na kuendeshea magari.
RC Zambi ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati na TPDC kwa kutenga fedha zitakazowezesha utekelezaji wa mradi huo katika Mkoa wa Lindi na baadae kote nchini.
Pia Mkuu huyo amewashukuru wananchi mkoani hapa kwa ushirikiano waliouonyesha katika kipindi chote cha kutekeleza mradi huo na kuwaomba waendelee na moyo huo wa kizalendo kwani mradi huo ni kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
More Stories
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi
Kampeni ya Sako kwa Bako yawafikia Kanda ya Kati