March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatangaza kupandisha kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imetangaza kupandisha kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi kutoka Shilingi 275,060 hadi Shilingi 358,322, ikiwa ni ongezeko la asilimia 33.4.

Hayo yamebainishwa Jijini Dar es salaam mapema leo Oktoba 17, 2025, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, amesema kuwa ongezeko hilo kwa sekta binafsi ni utekelezaji wa matakwa ya kisheria.

Ridhiwani, amesema mapitio ya kima cha chini cha mshahara hufanyika kila baada ya miaka mitatu, ambapo tangazo la mwisho lilitolewa mwaka 2022.

Amesema kuwa Serikali inataka waajiri wote wa sekta binafsi kuhakikisha wanazingatia na kutekeleza kima hicho kipya cha mshahara kwa mujibu wa sheria.

Aidha ametoa onyo kuwa Ofisi yake haitasita kuchukua hatua kwa waajiri watakaokaidi au kushindwa kutekeleza agizo hilo kwa makusudi, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wake.

“Ofisi yangu itaendelea kufatilia kwa karibu utekelezaji wa amri hii, kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi pamoja na kufanya tathimini ya mara kwa mara ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kikamilifu,” amesema

Aidha amesema kima hicho kipya cha mshahara kitaanza kutumika rasmi Januari 1, 2026, kikilenga kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na kuleta uwiano na ongezeko la mishahara ya watumishi wa umma lililotangazwa awali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara kwa Sekta Binafsi Dkt. Suleiman Rashid Mohamed amesema mchakato wa majadiliano ulikuwa shirikishi ambapo vyama vya wafanyakazi, waajili na waajiliwa vilishiriki kikamilifu katika hatua zote.

Naye Naibu Katibu Mkuu Shirikishio la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Rehema Ludanga amesema kitendo cha Serikali kutangaza Amri ya kupanda kwa mishahara kwa kima cha chini cha sekta binafsi ni faraja kwa wafanyakazi nchini kwani kimeonesha dhahili namna Serikali inavyothamini maslahi ya wafanyakazi nchini.

Rehema amesema kuwa ni wakati sasa waajiri wote katika sekta binafsi kutekeleza amri hiyo kwa kupandisha mishahara ikibidi zaidi ya kiwango kilichotangazwa ili kuongeza maslahi bora ya wafanyakazi wao.

Naye Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzan Ndomba amesema ATE ilishiriki kikamilifu katika mchakato wa maandalizi ya kima hicho kupitia kamati ya kitaalamu iliyozunguka mikoa mbalimbali.

“Kamati hiyo ilijumuisha waajiri, wafanyakazi na maofisa wa serikali. Pia tuliwapatia waajiri madodoso maalum ili kutoa maoni yao,” amesema Ndomba.