January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatambua mchango wa wanawake sekta ya uvuvi

Na Mwandishi wetu,timesmajira,Kigoma

Serikali imesema wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika kusimamia rasilimali za uvuvi pamoja na kuhakikisha biashara ya mazao ya uvuvi inaimarika ndani na nje ya Nchi.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia masuala la Udhibiti Ubora wa Mazao ya Uvuvi na Masoko, Steven Lukanga kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah wakati akizindua Mtandao wa Wanawake, Wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi Tanzania (TAWFA), Kanda ya Ziwa Tanganyika.

Amesema mchango huo wa wanawake unastahili kupewa thamani kubwa hasa katika kuweka mikakati ya kusimamia changamoto zao ikiwemo kuanzisha Dawati la Jinsia la Uvuvi Wizarani ili shughuli za masuala ya wanawake ziweze kuratibiwa.

“Ninatambua kuwa wanawake wamejiunga katika vikundi mbalimbali ambavyo vinarahisisha utendaji wa shughuli zao za uvuvi na shughuli nyingine katika mnyororo wa thamani, pamoja na hayo vikundi hivi vinakabiliwa na changamoto kama upatikanaji wa masoko, taarifa mbalimbali za bei ambapo shughuli zao zina kuwa ngumu, ”Amesema Lukanga.

Pia amesema Wizara imeweka juhudi katika kutatua changamoto mbalimbali za wadau wa Sekta ya Uvuvi ili kuongeza mchango wa Sekta kwenye uchumi wa nchi ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara za mazao ya uvuvi, kuzuia uvuvi haramu, kuzuia utoroshwaji holela wa rasilimali za uvuvi, na kuwezesha uvuvi endelevu.

“ Juhudi hizi zinalenga kuwezesha wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi ambao 50% ni wanawake ili waweze kuhimili ushindani wa kibiashara ndani na nje ya nchi na nipende kushukuru Shirika la FAO kupitia Mradi wa Fish4ACP unaotekeleza mradi na kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi katika Ziwa Tanganyika,”amesema.

Naye Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia uendelezaji wa rasilimali za uvuvi ,Merisia Palazo amesema wanawake wote wanaojishughulisha katika mnyororo wa Uvuvi wanatambulika na ndio maana kukawa na jukwaa linalowawezesha kuelezea mambo yao mbalimbali yanayowakabili.

Vilevile Mratibu wa Sekta ya Uvuvi Kitaifa kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO),Oliva Mkumbo amesema lengo la kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia uvuvi ili kuinua kipato cha familia na kuondokana na umasikini.

“Kutokana na mchango mkubwa wa kina mama katika shughuli za kiuchumi mradi huo unalenga kumgusa kila mwanamke na kama shirika litaendelea kufungua matawi katika maeneo mbalimbali na hatimaye sekta ya uvuvi kuwa yenye tija,” amefafanua Mratibu huyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanawake wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi Tanzania (TAWFA), Kitaifa Beatrice Mmbaga amesema kuwa kuzinduliwa kwa jukwaa hilo ni sehemu ya kutatua changamoto zinazowakabili kina mama katika nyanja ya uvuvi.