September 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatakiwa kushirikiana na asasi kutoa elimu ya mabadiliko ya tabia nchi

Na Jovither Kaijage,TimesMajira,Online Ukerewe

WAKAZI wa Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza wameomba Serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya serikali kuchukua hatua madhubuti hasa kwa kuelimisha jamii juu ya tatizo la mabadiliko ya tabia nchi kama mkakati wa kukabili tatizo hilo linaloendelea kuongezeka na kuleta madhara kwa maisha ya watu na mali.

Ombi hilo imetolewa juzi na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bukongo na wananchi wa Kijiji cha Bukongo kwenye mafunzo kuhusiana na namna ya kukabili tatizo hilo.

Mafunzo hayo yalitolewa wiki hii na Shirika la Sauti ya Wanawake Ukerewe (SAWAU) kwa kushirikiana na Shirika la Women Action Towards Economic Development (WATED) kwa ufadhili wa Global Alliance for Green And Gender Action na BothENDs (GAGGA) ya nchini Uholanzi.

Mmoja wa wanafunzi hao, Emanuel Jovin alipongeza hatua hiyo na kuahidi kuelimisha jamii inayomzunguka juu ya tatizo la uhalibifu wa mazingira unaosababisha tatizo la tabia nchi.

Amesema kama jamii itaelimishwa kwa kiwango cha kutosha inaweza kushiriki kikamilifu kuendesha shughuli zao kwa kuzingati ulinzi wa mazingira, hatua hiyo itapunguza madhara ya tabia nchi kama vimbunga, ukame na magonjwa ya binadamu na mimea.

Akifafanua zaidi amesema mbali ya kuelimishwa sababu za tatizo hilo, pia alipata taarifa za kitaalamu za hali ya hewa msimu huu wa kilimo, ambapo Mamlaka ya Hali ya Hewa ilitoa taarifa inayoonesha msimu huu wa kilimo wa 2021 mvua zitanyesha chini ya wastani, hivyo kushauri wakulima kulima mazao yanayoimili ukame kama mtama, viazi vitamu na mihogo

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bukongo Kati, Masumbuko Masyeba amesema mafunzo hayo yamemjengea uwezo wa kutimiza wajibu wake vyema hasa kwa kusimamia ulinzi wa mazingira katika eneo lake.

Amesema mbali ya kusimamia matumizi mazuri ya ardhi kwa weledi katika Kijiji cha Bukongo, pia hatatoa elimu kwa jamii juu matumizi ya nishati mbadala kama majiko banifu na gesi hivyo kulinda mistu.

Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Isack Mgendi mbali ya kubainisha sababu za kuwepo tatizo la tabia nchi pia aliwaimiza wakulima wa wilaya hiyo msimu huu wa kilimo kulima mazao yanayostaimili ukame kwa sababu mvua zitanyesha chini ya wastani.

“Ndugu zangu tumeona sababu na njia za kuepuka tatizo la tabia nchi , lakini nitumie fursa hii kuwafahamisha kuwa taarifa za awali zilizotolewa na mamlaka ya hali ya hewa msimu huu wa kilimo zionesha mvua zitanyesha chini ya wastani, hivyo ni vema wakulima tufuate maelekezo ya wataalamu kulima mzao yanayostaimili ukame pamoja na kutumia vizuri akiba ya chakula tulichonacho ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na tatizo hilo.

“Tukiepuka kukata miti na kufuga mifugo kwa kuzingati ukubwa wa ardhi tuliyonayo, kilimo cha kinga maji na kuepuka kuchoma moto nyika na mistu yetu inaweza kuwa kinga ya tatizo la tabia nchi,”amesema.

Mwezeshaji wa Shirika la SAWAU, Leocadia Vedastus alisema lengo la mradi huo ni kushirikisha viongozi na jamii kutambua na kukabili madhara ya tabia nchi kama mkakati wa kupunguza umaskini na magonjwa kama utapiamlo.