November 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatakiwa kujenga vituo vya afya pembezoni mwa miji

Na Penina Malumdo,timesmajira,Online

CHAMA cha Mapinduzi CCM, kimeitaka Serikali kujenga vituo vya Afya kwenye maeneo ya pembezoni kwa lengo la kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi wanaoishi maeneo hayo.

Pia Vituo hivyo vitakavyojengwa vinatakiwa visijengwe karibu karibu kama sehemu za maonesho bali vijengwe kwa lengo kutatua changamoto ya Wananchi.

Akizungumza hayo leo wilayani Masasi Mkoa wa Mtwara,Katibu Mkuu wa CCM,Daniel Chongolo wakati wa ziara ya Sekretarieti ya CCM Taifa ya Kukagua utekelezaji wa ilani na Uhai wa Mashina ya Chama hicho.

Amesema ni lazima vituo vya afya vijengwe karibu na maeneo hayo ya wananchi lengo ni kuhakikisha huduma ya afya inafikia kwa ukaribu kwao.”Serikali kazi yake ni kutoa fedha ila nyie viongozi kazi yenu simamieni utekelezaji,”alisema

Chongolo amesema ni vema kuwepo kwa huduma nzuri ya mama na mtoto kwani mama wanapopata ujauzito awe na mahali yenye adhi ya kwenda kujifungulia.

“Mama anapaswa kujifungulia sehemu nzuri kama tukio analoenda kufanya la kuleta kiumbe mwingine Duniani,tusipokuwa na vituo vya afya au zahanati zilizokaribu na maeneo tunayoishi ni ngumu sana kuwa na uzazi salama,”amesema

Aidha amesema Serikali imeweka mpango ambapo mwaka huu zimetolewa fedha kwaajili ya kujenga vituo vya afya 250 na mwezi Oktoba mwaka huu kuna fedha nyingine zinazotarajiwa kutolewa kwa vituo vingine 250.”lengo ndani ya mwaka huu serikali ijenge takribani vituo 500vya afya ndani ya nchi yetu yote,”amesema

Chongolo amewahasa wananchi wa Wilaya hiyo kuacha kujifungulia nyumbani badala yake waende kwenye vituo vya afya na zahanati ndiko kwenye uhakika wa kupata huduma bora ya afya