January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yataka siku moja kila mwezi kuchunguza saratani nchini

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amemuagiza Katika Mkuu wa Wizara hiyo kuhakikisha anaweka utaratibu na kutenga angalau siku moja kwa mwezi nchini kote ambayo itatumika kwa ajili ya kutoa huduma za uchunguzi wa saratani kwa wananchi.
Akizungumza jijini Dodoma katika kituo Cha Afya Makole kwenye maadhimisho ya siku ya saratani Duniani, Ummy amesema hatua hiyo itasaidia kuwabaini watu wenye dalili za Awali za saratani na kuwapatia tiba mapema na hatimaye kupunguza ongezeko la wagonjwa wa saratani nchini.
Maadhimisho ya siku ya saratani Dunia hufanyika Februari 4, ya kila mwaka Duniani kote ambapo maadhimisho hayo mwaka huu yanaongozwa na  kauli mbiu isemayo’huduma ya saratani sawa kwa wote’ambayo inamtaka kila mtu kwa nafasi yake kushiriki katika mapambano dhidi ya saratani.
Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa Saratani 42,060 kwa mwaka na kwamba  takribani wagonjwa 28,610 sawa na asilimia 68 wanapoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.  
“Idadi hii ni kubwa,kwa hiyo tukiweka utaratibu huu wa kutenga angalau siku moja kwa mwezi kufanya uchunguzi wa watu ,itasaidia kugundua maambukizi ya saratani katika hatua za Awali na hivyo kuwatibu na kupona kabisa.”amesema Ummy 
Aidha kwa mujibu wa  taarifa za mwaka 2021 kutoka kanzi data ya wagonjwa iliyopo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road inaonesha kuwa Saratani zinazoathiri wanaume zaidi ni pamoja na saratani ya tezi dume  (21%), Saratani ya Koo (11.8%),Saratani ya utumbo mkubwa na mdogo (9%) na Saratani ya mdomo na kinywa (7.3%)huku kwa upande wa wanawake wanaathiriwa zaidi na  Saratani ya Mlango ya Kizazi (43%), Saratani ya Matiti (14.2%) na Saratani ya koo (3.8).
“Kwa hiyo kama tunavyoona saratani ya mlango wa kizazi inawaathirinwanawake kwa asilimia 43 ,kwa hiyo tukifanya uchunguzi mapema tukaidhibiti saratani yalango wa kizazi kwa wanawake mapema Ina maana tutapunguza saratani kwa zaidi ya asilimia 40.”amesisitiza Waziri huyo
Ametaja mambobalimbali yanayochangia ongezeko la wagonjwa wa saratani ni pamoja  na magonjwa mengine yasiyoambukiza ambayo huchangiwa zaidi na mtindo wa maisha usiozingatia lishe bora , kutokufanya mazoezi (Tabia Bwete), unene uliokithiri, matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, matumizi ya pombe kupita kiasi na ulaji usiofaa kama kutokula mbogamboga na matunda, matumizi ya chumvi na sukari kwa wingi,”amesema.
“Katika kipindi cha  miaka 10 iliyopita, Tanzania imeshuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani zinazochangiwa na mtindo wa maisha ikilinganishwa na ilivyokuwa awali ambapo wagonjwa wengi walikuwa ni wale wenye saratani zinazotokana na maambukizi ya virusi”
Amesema kwa  kutambua hilo, Serikali imeongeza juhudi za kuhakikisha kuwa uelewa katika jamii kuhusiana na tatizo hili unaongezeka kwa kuandaa mtaala wa mafunzo mashuleni unaozungumzia magonjwa yasiyoambukiza na namna ya kudhibiti na kuanzisha Program ya taifa ya kuzuia na kudhibiti magonjwa Yasiyoambukiza  yasiyoambukiza ikiwemo saratani.
Waziri Ummy amewasihi wananchi wote wakiwemo wanawake na wanaume kila mmoja kwa nafasi yake kwenda kupima saratani ili kupata tiba mapema kwa watakaogunduluka kuugua.
“Wanawake wenzangu naomba tujitokwze kwa wingi kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi,lakini na ninyi wanaume jitokezeni kupima saratani ya tezi dume muache uoga kwenda kupima ,siku hizi Kuna njia za kisasa kabisa kupima saratani ya tezi dume.”