Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Tabora
SERIKALI imezielekeza kampuni za uchimbaji madini kuhakikisha wanaendelea kushiriki katika shughuli za kijamii ili kujenga mahusiano mazuri na wananchi wanaozunguka maeneo ya migodi.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tabora Mhandisi, Abel Madaha wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu fursa mbalimbali zitokanazo na sekta ya madini katika Mkoa huo.
Amesema Tume ya Madini imepewa jukumu la kusimamia sheria ya madini katika kifungu cha 22 na kuhakikisha sekta hiyo inatoa mchango wake katika pato la Taifa.
“Tunatoa wito kwa kampuni zote za uchimbaji kuhakikisha zinashiriki katika shughuli za kijamii kwa kurudisha faida ya mapato wanayopata ili kujenga mahusiano mazuri na Wananchi wanaozunguka migodi,”amesema Madaha
Mhandisi Madaha pia amesisitiza kampuni za uchimbaji wa madini kuhakikisha zinatoa kipaumbele cha ajira kwa Watanzania wazawa ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
“Nichukue fursa hii kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka miundombinu wezeshi katika sekta ya madini hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi utokanao na sekta hiyo na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa hadi kufikia asilimia 9,”amesema.
Kwa upande wake Mratibu wa Miradi wa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya TAUR Tanzania Limited, Edith Moses amesema katika kuhakikisha wanatekeleza sheria ya madini tayari wamejenga madarasa mawili na vyoo katika shule ya Msingi na Sekondari Nanga iliyopo Wilaya ya Igunga.
Naye Mwendesha mitambo wa Kampuni ya TAUR Tanzania amesema uwepo wa machimbo umesaidia kutoa ajira kwa vijana wengi ambapo sasa wanapata fedha ambazo zinawasaidia kuhudumia familia zao.
“Tunaishukuru Tume ya Madini kwa kusimamia sheria mbalimbali zilizowekwa katika maeneo ya machimbo ambapo sasa usalama unazingatiwa na vijana wengi wazawa wameajiriwa.
More Stories
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi