January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yasikia kilio cha wananchi kuhusu tozo za miamala ya simu

Na Benny Mwaipaja,TimesMajira Online, Dar

WAZIRI wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesema Serikali imesikia kilio na maoni ya wananchikuhusu tozo mpya ya miamala ya simu na kuwaomba wawe watulivu wakati jambo hilo linatafutiwa ufumbuzi.

Dkt.Nchemba ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo vya habari akiambatana na Waziri wa Teknolojia ha Habari na Mawasiliano Dkt. Faustine Ndugulile.

“Kwa maaneo ambayo wananchi wametoa ushauri na kuelezea namna ambavyo jambo hili linawagusa lakini pia tumepokea maeneo ambayo yanatakiwa kutoa elimu zaidi ili kujenga uelewa wa pamoja ikiwa ni pamoja na viwango vinavyokatwa kwa nayetuma na anayetoa lakini pia kuhusu mantiki ya jambo lenyewe” amesema Mwigulu.

Amesema kuwa jambo la tozo za miamala linatekelezwa kupitia sheria iliyopitishwa na Bunge lakini kuna kanuni za utekelezaji zinazomhusu yeye kama Waziri wa Fedha na Mipango na maeneo mengine yanahusu Wizara ya Teknollojia ya Habari na Mawasiliano ambazo zitajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.

Dkt. Nchemba amesema kuwa kesho kutakuwa na kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, kujadili suala hilo na pia kutakuwa na kikao kingine cha Mawaziri wa Wizara zote kuchambua kwa kina suala hilo.