November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yashauriwa kufanya mapitio ya sera

Na Bakari Lulela

SERIKALI imeshauriwa kufanya mapitio ya sera miongozo ya uzalishaji pamoja na kuongeza jitihada za kuelimisha jamii, masuala ya sekta ya uwekezaji wa kilimo likiwa na lengo la kusaidia kuepukana na janga la uhaba wa chakula nchini.

Ushauri huo umetolewa mkoani Dar es Salaam katika kikao cha wadau wa chakula na Mwenyekiti wa Wabunge Vinara wa Usalama wa Chakula (FoodSafety) Mbunge wa Viti Maalumu, Neema Lugangira ambapo amesema serikali haina budi kuboresha mifumo ya chakula kuanzia kwa wazalishaji, watunzaji kwenye maghala na walaji kwani chakula lazima kiangaliwe ili afya ziwe bora.

Amesema Tanzania bado kuna baadhi ya maeneo yanakabiliwa na uhaba wa chakula, kitu kinachosababisha watoto wengi kuwa na udumavu na utapiamlo katika ukuaji wao, kutokana na vyakula wanavyokula hivyo kupitia kikao hicho na Mkutano Mkuu wa Chakula, unaotararajiwa kufanyika Septemba mwaka huu Jijini New York, Marekani wawakilishi watakaokwenda watakuja na suluhisho.

Naye Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mazingira, Clara Makenya amesema wakati wa sasa kilimo kimekuwa kikiyaathiri mazingira kutokana na wakulima wengi, matumizi ya dawa na viatilifu kwa wakulima wengi hali inayosababisha, ardhi kupoteza mbolea yake ya asili siku hadi siku kusababisha mazingira kuharibika huku uzalishaji ukipungua kwa kiasi kikubwa, hivyo mdahalo huo utaibua taswira chanya kwa namna bora ya kilimo chenye tija, kisicholeta athari kwa mazingira na afya kwa wanadamu.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Kassim Khaji amesema hali ya usalama kwa chakula upande wa Zanzibar iko salama ingawa si kwa kiasi kikubwa, kwani katika kipindi cha janga Covid-19, ilikabiliwa na uhaba wa chakula na kusababisha kuagiza na kusaidiwa chakula kutoka nje ya nchi.