November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yasaini mikataba mitatu ujenzi kituo kikuu cha mabasi, barabara za mitaa

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

SERIKALI kupitia Wakala wa barabara za Mjini na Vijijini (TARURA)mkoa wa Mbeya imesaini mikataba mitatu kwa pamoja ya ujenzi wa kituo kikubwa cha mabasi chenye uwezo wa kuchukua mabasi 120 kitakachokwenda kutatua changamoto ya wananchi kukosa kituo maalum cha mabasi yaendayo Mikoani.

Pia utiaji saini wa mikataba hiyo utahusisha barabara za mitaa kwa kiwango cha Lami na ujenzi wa soko la kisasa la Sokomatola ambao thamani yake ni shilingi Bil.30 lengo likiwa ni kuboresha huduma na miundombinu kwenye jamii.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo la utiaji saini Mikataba hiyo mitatu Julai 27,2024 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Mohamed Mchengerwa amesema kuwa lengo ni kuboresha miundombinu katika Miji,Manispaa na Majiji (TACTIC).

Aidha Mchengerwa amesema kuwa mikakati hiyo ujenzi wa stendi na soko pamoja na barabara havijaja kwa bahati mbaya katika mkoa wa Mbeya bali ni sababu mkoa umepata Mbunge ambaye anawaletea maendeleo.

Aidha Waziri Mchengerwa amesema kuwa Wizara yake imepokea maelekezo mahususi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha inatekeleza maombi yote yaliyotolewa na Mbunge wa Jimbo hilo Dkt. Tulia ya kuhakikisha inazitatua changamoto zote zikiwemo za barabara, elimu,afya .

Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge Dkt.Tulia Ackson ameishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio cha wananchi wa Mbeya kwa hatua ya kuanza kuboresha miundombinu mbalimbali katika Jiji la Mbeya ikiwemo barabara ambazo zimekuwa kero kwa miaka mingi.

Hata hivyo Dkt.Tulia amesema kuwa, pamoja na Jiji hilo kuwa na changamoto nyingi suala la barabara limekuwa kikwazo zaidi kutokana na maeneo mengi kutopitika ikiwemo barabara za mitaa hivyo kurudisha nyuma shughuli za maendeleo kwa wananchi.

Aidha Dkt.Tulia amebainisha kuwa baada ya kutoa kilio hicho cha wananchi tayari Serikali imekwishaanza kufanyia kazi maeneo mbalimbali kwa kujenga barabara za mitaa kwa kiwango cha lami ikiwemo barabara kuu ya njia nne Igawa-Ifisi.

Kwa upande wake Waziri Mchengerwa amesema kuwa Wizara yake imepokea maelekezo mahususi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha inatekeleza maombi yote yaliyotolewa na Mbunge wa Jimbo hilo Dkt.Tulia ya kuhakikisha inazitatua changamoto zote zikiwemo za barabara, elimu, afya .

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa barabara za Vijijini na mjini (TARURA) Mhandisi,Victor Seif amesema mpango huo ni mkakati wa kutatua changamoto za miundombinu ya barabara za mitaa nchini.

Mhandisi Seif amesema kwamba malengo ya mradi huo ni kuboresha miundombinu ya halmashauri 45,ambazo ni Majiji matano , Manispaa 16 na Miji 24 na kusema kuwa kwenye halmashauri 45 zitajengewa uwezo ili kuweza kujiimarisha katika usimamizi na uendelezaji wa Miji pamoja na ukusanyaji mapato.