December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yapongezwa manufaa ya WCF kwa watumishi wa umma, binafsi

K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, MWANZA

MADAKTA wameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wake Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka mazingira rafiki na mazuri kuhakikisha Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) unatekeleza malengo yake ya ulipaji wa fidia kwa wafanyakazi wanaoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.

Wameyasema hayo jijini Mwanza mwishoni mwa kikao kazi kilichoandaliwa na WCF kuwajengea uelewa madaktari kutoka mikoa ya Kanda ya ziwa kuhusu namna ya kufanya tathmini ya ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi.

“Napenda kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka mazingira rafiki na mazuri kuhakikisha WCF inaweza kutekeleza malengo yake kwa maana ya kuhudumia watumishi wa sekta ya umma na sekta binafsi wanaoumia au kuugua kutokana na kazi.” Alisema Dkt. Pasclates Ijumba kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.

Alisema mafunzo hayo yamewawezesha kuelewa kuwa madaktari wanahusika katika mchakato wa kusaidia WCF kulipa fidia stahiki kwa kufanya tathmini sahihi

“Nitakachokisaidi kwa Mfuko ni kuhakikisha nafanya tathmini ya kina kwa mgonjwa ili aweze kupata stahiki zake lakini bila kuuonea Mfuko.” Amesema Dkt. Charles Makoye kutoka Hospitali ya Wilaya Maswa.

Naye Dkt. Noel Saitoti kutoka Hospitali ya Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera alisema licha ya ukweli kwamba WCF ina muda mfupi wa miaka minane tangu kuanzishwa kwake lakini imeshakuwa role model (mfano wa kuigwa) kutokana na mifumo yake mizuri ya utoaji huduma na kuzipita nchi nyingi za Afrika zilizotangulia muda mrefu kwenye sekta ya utoaji fidia kwa wafanyakazi.

Alisema mafanikio hayo kwa kiasi kikubwa yametokana na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wake Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kupitia Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu inayosimamia Mfuko huu, imeuwezesha Mfuko kutekeleza vema majukumu yake.

“Nimesoma kwenye vyombo vya habari kwamba Afrika Kusini, Kenya na Zambia zimekuja Tanzania kujifunza kutoka WCF, hii ni heshima kubwa kwaMfuko lakini kwa nchini yetu.” Alisema Dkt. Saitoti.

Aidha madaktari hao pia wameipongeza WCF kwa namna inavyotumia teknolojia (TEHAMA) kurahisisha utoaji wa huduma.

“Mchakato wa utoaji taarifa unaishia online, mwajiri hahitaji kwenda ofisi za WCF anachotakiwa ni kuingia kwenye mfumo na kutuma taarifa ya tukio WCF na Mfuko unapata taarifa siku hiyo hiyo ya tukio.” Amesema Dkt. Raphael Kibata kutoka Hospitali ya Wilaya Butiama.

Akizungumza wakati wa kuahirisha kikao kazi hicho, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana, aliwaasa madaktari hao kuzingatia maadili ya kazi zao wanapotekeleza wajibu wa  kufanya tathmini ya ulemavu (Impairment Assessment) kwa wafanyakazi walioumia au kuugua kutokana na kazi.

“Kwa kufanya hivyo mtausaidia mfuko kutoa fidia stahiki na kwa wakati, ninaamini mkifika kwenye maeneo yenu mtaenda kufanya kwa vitendo” Alisema.

Alisema Mfanyakazi akiwa na uhakika wa kinga ya kipato chake atafanyakazi kwa bidii na kujituma kwani anajua hata akiumia kiko chombo kitakachosimamia maisha yake na familia yake.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu WCF, Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF, Dkt. Abdusalaam Omar alisema Mafunzo hayo yamejikita kwenye maeneo makubwa mawili ambayo ni pamoja na kuwawezesha madaktari kuweza kubaini magonwja yatokanayo na kazi.

“Sehemu ya pili ni kuwawezesha madaktari kufanya tathmini ya ulemavu wa kudumu na kujua mfanyakazi aliyeumia au aliyepata ugonjwa unaotokana na kazi ana asilimia ngapi kutokana na madhara aliyoyapata.” Alifafanua.

Madaktari walioshiriki kikao kazi kilichoandaliwa na WCF kuwapatia mafunzo ya tathmini za ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi jijini Mwnaza, wakionyesha stika watakazobandika kwenye maeneo yao ya kazi kuonyesha wataalamu wa tathmini wanapatikana kwenye maeneo yao ya kazi.
Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini (WCF), Dkt. Abdulsalaam Omar akizungumza kwenye mafunzo hayo
Dkt. Pascal Magesa, Afisa Tathmini Mwnadamizi WCF
Dkt.Robert Mhina, Bingwa na Mbobezi w amagonjwa ya Mifupa akionyesha jinsi ya kufanya tathmini kwa kutumia kipimo cha Goniometer.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano WCF, Bi. Laura Kunenge (kulia) akimkabidhi stika, mshiriki kutoka Shinyanga, Dkt. Mariaconsolata kama ishara ya kukamilika mafunzo. Stika hizo zitatumika kubandikwa kwenye hospitali wanakotoka washiriki ili kuonyesha kuwa Wataalamu wa Tathmini wanapatikana  kwenye hospitali husika.
Mgeni rasmi 

Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana

 akikabidhi cheti mmoja wa wahitimu wa mafunzo.