Na Mwandishi Wetu, TimesMajira, Online Kahama
KATIBU Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya amewapongeza wananchama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahama (Kahama Cooperative Union Ltd – KACU) kwa kuzindua rasmi kiwanda cha kuchakata pamba.
Hafla ya uzinduzi huo ilioongozwa na Naibu Waziri Kilimo, Hussein Bashe, jana katika mji wa Kahama.
Kusaya amesema wanachama wa Chama Kikuu cha KACU Ltd wanastahili pongezi nyingi kwa kuwa mazingira hayakuwa rahisi kufufua kiwanda hicho na kuongeza kuwa vyama vikuu vingine vinastahili kuiga mfano huo.
Chama Kikuu cha Ushirika cha KACU Ltd kimefanikisha jambo hili baada ya kuandaa mpango biashara kwa ajili ya kufanya shughuli za uchakataji wa pamba ambapo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kupitia mpango huo, Iliridhia kukikopesha Chama hicho, mkopo wa jumla ya sh. Billioni 4 ili kufanya ukarabati wa kiwanda, ununuzi wa pamba mbegu na uchakataji wa pamba mbegu ili kuzalisha pamba nyuzi na pamba mbegu.
Aidha, Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa Chama Kikuu cha Ushirika cha KACU Ltd kilisajiliwa mwaka 1994 kwa hati ya usajili namba 5,493 ambapo wakati hadi sasa kina jumla ya vyama wanachama 116 na kwamba kufufua mashine hizo ambazo zilisimama tangu msimu wa kilimo wa mwaka 2013/2014 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uzalishaji mdogo wa pamba pamoja na kushindwa kuhimili ushindani wa makapuni binafsi.
Ameongeza kuwa uanzishwaji wa kiwanda hicho; Uende sambamba na ongezeko la uzalishaji wa pamba na tija.
“Ndugu zangu wanaushirika na Wakulima, ili kiwanda kiendelee kijiendeshe kwa tija ni lazima tuzalishe malighafi za kutosha, maana yake ongezeni uzalishaji wa pamba mara mbili ya uzalishaji wa mwaka huu, na anzeni kwa kutumia mbegu bora, tumieni mbolea na Watumieni Wataalam wote, wakiwepo Maafisa Ugani”.Alisema.
Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa ili kiwanda kiendelee vizuri ni lazima pamba izalishwe kwa wingi ili kukifanya kiwanda kijiendeshe kwa kipindi cha mwaka mzima.
“Ninyi wote ni mashahidi kuwa baada ya mavuno ya pamba kuisha, viwanda vyetu wa vinafanya kazi kwa kipindi kifupi cha miezi miwili hadi mitatu; Hii si sahihi ni vizuri viwanda vikaongeza usindikaji kwa kipindi kirefu cha mwaka mzima; kuwa na kiwanda kama hiki cha Kahama chenye uwezo mkubwa wa kusindika pamba nyingi zaidi ya kilo elfu 71 kwa siku.” Amesema Kusaya.
Kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata pamba mbegu kilo 68,825 hadi 71,693 kwa siku na kuzalisha robota 144 hadi 150 za pamba nyuzi. Uwezo huo ni mkubwa na ambao unaweza kuchakata pamba zote zinazozalishwa katika mkoa wa Shinyanga kwa zaidi ya kilo 6,100,000 kwa msimu mzima.
Katibu Mkuu kusaya ameongeza kuwa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuanzisha, kuendeleza na kufufua viwanda ambavyo vilikua havifanyi kazi kwa muda mrefu na kwamba kuanza kufanyakazi kwa kiwanda hicho ni juhudi ya Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na Benki ya Kilimo (TADB) baada ya kuja na mpango wa kuanza kufufua viwanda vilinavyomilikiwa na Vyama vya Ushirika katika zao la pamba vilivyopo katika Mikoa ya Geita na Shinyanga.
Wakati huo huo Katibu Mkuu ametumia muda huo kutoa onyo kwa Wabadhilifu wote wa mali za ushirika popote nchini kuhakikisha wanarejesha mali za Wanachama wa Ushirika mapema kabla Serikali haijachukua hatua.
Katibu Mkuu Kusaya amesema mali zote zilizoibwa na kuporwa na Viongozi wachache wasio waaminifu, zitarejeshwa kama ambavyo zimeendelea kurejeshwa maeneo mbalimbali kote nchini.
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani