Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Daudi amesema, tangu kuanzishwa kwa mfumo wa kielektroniki wa kupokea, kufuatilia na kushughulikia malalamiko (e-Mrejesho) kumekuwa na mwitikio chanya wa wananchi na watumishi wa umma kuutumia mfumo huo, ambao umeiwezesha Serikali kupokea na kushughulikia kwa wakati jumla ya maoni na malalamiko 239,196 yaliyowasilishwa katika Taasisi za Umma.
Daudi amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya matumizi na uendeshaji wa mfumo wa kutuma, kupokea na kufuatilia malalamiko, mapendekezo, maulizo na pongezi (e-Mrejesho) kwa Maafisa Malalamiko na TEHAMA wa Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara, Wakala na Idara Zinazojitegemea ambao wamepewa dhamana ya kushughulikia malalamiko kwenye taasisi zilizopo kanda ya mashariki.
Daudi amesema kuwa, miaka ya nyuma kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo wa kielektroniki haikuwa rahisi kushughulikia malalamiko kwa wakati na kuwa na takwimu halisi za maoni na malalamiko yaliyofanyiwa kazi ambazo zinatumiwa na Serikali kama mrejesho wa kuboresha huduma zinazotolewa na Taasisi za Umma kwa wananchi.
Aidha, Daudi ameeleza kuwa, Ofisi ya Rais – UTUMISHI kupitia Idara ya Ukuzaji Maadili imejipanga kuendelea kutoa mafunzo kwa Maafisa Malalamiko na TEHAMA katika taasisi zote za umma nchini, ili kuwajengea uwezo wa kutumia vema mfumo huo wa kieletroniki kushughulikia malalamiko yote yanayowasilishwa na wananchi na wadau kwa wakati.
Daudi ameongeza kuwa, Mfumo wa e-Mrejesho umesanifiwa kwa namna ambayo inaongeza uwazi, uwajibikaji na usikivu kwa watendaji Serikalini, kwani mfumo unawawezesha viongozi katika ngazi mbalimbali kuona na kufuatilia namna ambavyo malalamiko au maoni yanavyoshughulikiwa.
“Endapo kutakuwa na ucheleweshwaji wa kutoa mrejesho au uzembe wa aina yoyote, mfumo unampa fursa kiongozi katika taasisi husika kuchukua hatua stahiki kwa wakati,” Bw. Daudi amefafanua.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best