Na Mwandishi Wetu, Simiyu
SERIKALI katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imeboresha miundombinu ya umwagiliaji nchini,hivyo kuongeza eneo linalomwagiliwa kutoka hekta 461,000 mwaka 2015 hadi kufikia hekta 694,715 mwaka 2020.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Maonesho ya NaneNane yanayofanyika mjini Simiyu, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Daudi Kaali amesema ongezeko hilo la eneo ambalo ni asilimia 50.7 limetokana na uboreshaji wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu mbalimbali za umwagiliaji nchini.
Kaali ameeleza kuwa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imefanikiwa kukarabati skimu 179 za umwagiliaji na hivyo kuongeza eneo linalomwagiliwa kufikia hekta 694,715 ambalo sehemu kubwa li zao la mpunga.
Amesema Kwa mujibu wa Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 (The National Irrigation Master Plan) Tanzania ina eneo la hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji.
Kati ya hekta hizo, hekta milioni 2.3 zinauwezekano mkubwa wa kumwagiliwa, hekta milioni 4.8 zinauwezekano wa kati na hekta milioni 22.3 zinauwezekano mdogo wa kumwagiliwa.
Hadi kufikia mwaka 2015 kabla ya kuanza kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, jumla ya hekta 461,000 zilikuwa zimeendelezwa kwa kilimo cha umwagiliaji.
Aliongeza kuwa lengo kuu la Tume ni kuendeleza kilimo cha umwagiliaji kwa kuzingatia matumizi bora ya rasilimali kwa lengo la kuwa na uzalishaji wenye tija na endelevu kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Alisema kati ya skimu zilizojengwa na kukarabatiwa, skimu 56 zimekamilika na zinasubiri kuzinduliwa. Mafaniko mengine aliyoyataja kuwa ni kuongezeka kwa tija ya uzalishaji katika skimu zilizoendelezwa, ambapo uzalishaji umeongezeka kutoka wastani wa tani 1.8-2.0 kwa hekta hadi kufikia wastani wa tani 4.0-5,0 kwa hekta kwa zao la mpunga.
Zao la mahindi uzalishaji wake umeongezeka kutoka tani 1.5 hadi tani 3.7-5.0 kwa hekta, vitunguu kutoka tani 13 hadi 26 kwa hekta na nyanya kutoka tani 5 hadi 18 kwa hekta.
Kaali alisema mafanikio hayo yamepatikana kwa kutekeleza miradi mbalimbali ukiwemo mradi umwagiliaji wa kuendeleza wakulima wadogo (Small Scale Irigation Development Project –SSIDP) ambao ulitekelezwa katika awamu tatu katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini.
Aidha akizungumzia mapema kuhusu mchango wa kilimo cha umwagiliaji katika uchumi wa nchi kuanzia mwaka 2015-2020, Mhandisi Daniel Manase anayeshughulika na kitengo cha ukaguzi na Udhibiti ubora wa miradi ya umwagiliaji alisema kuwa kilimo cha umwagiliaji kimechangia asilimia 24% ya upatikanaji wa mazao ya chakula nchini.
Mhandisi Manase amesema kilimo cha umwagiliaji kimesaidia sana kupunguza ile fedha ambayo ingetumika kuagiza chakula kutoka nje ya nchi kwa hiyo inakwenda kwenye shughuli nyingine za maendeleo.
Ameongeza kuwa pamoja na hilo kilimo hicho kimeweza kuchangia kutoa ajira kwa wananchi’’ Alisema Mhandisi Manase.
Aidha Kaimu Mkurugenzi wa Usanifu na Utafiti Mhandisi Gregory Chigwiye akiongelea mikakati ya Tume hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo 2020-2025, amesema Tume imejipanga kujenga na kuboresha miundombinu ya umwagiliaji ili kufikia eneo la umwagiliaji linalofikia hekta 1,000,000.
More Stories
TARURA Kilimanjaro yatimiza ahadi ya Rais Samia
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria
Wananchi wakubali yaishe Bangi kubaki historia Tarime