January 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaombwa kuanzisha masoko maalum ya alizeti

Na Nathaniel Limu,TimesMajira online,Singida

SERIKALI imeombwa kuangalia uwezekano wa kuanzisha masoko maalum ya kuuzia alizeti,ili mkulima na serikali, iweze kupata malipo/tozo stahiki.

Meneja wa kiwanda cha Mount Meru,Nelson Lutengano Mwakabuta, akitoa taarifa kuhusu uendeshaji wa kiwanda hicho kikubwa Afrika Mashariki kwa waandishi wa habari juzi. Kulia ni mkulima maarufu wa zao la alizeti mkoani Singida,Mihammed Iddi.Picha na Nathaniel Limu.

Wito huo umetolewa juzi na meneja wa kiwanda cha Maount Meru, Nelson Lutengano Mwakabuta,na kusema kuanzishwa kwa masoko hayo,kutasaidia kwa kiwango kikubwa kukomesha walanguzi kuendelea kuwanyonya na kuwadhulumu wakulima.

Amesema sasa wakati umefika,zao ka alizeti liwe na masoko katika kila kijiji,ili wanunuzi wawe ni wanaoeleweka na washindane bei katika kununua alezeti.

Meneja huyo amesema masoko hayo ambayo yatakuwa kisheria,yatakuwa na mizani halali ya kupimia alizeti.Pia yatakuwa na chekecheo kwa ajili ya kusafisha mbegu ya alizeti.

“Kupitia masoko hayo wakulima wataanza kunufaika na kilimo chao cha alizeti.Malengo yao yatafikiwa kwa vile watapata malipo yanayofanana na thamani ya alizeti iliyouzwa.Serikali nayo itapata tozo stahiki”,amesema meneja huyo.

Aidha,amesema kuwa wakulima baada ya kudhulumiwa na walanguzi kwa miaka mingi,sasa ari yao ya kulima alizeti imepungua mno.Msimu huu,alizeti imelimwa kidogo na haitakidhi mahitaji ya viwanda vilivyopo.

“Kazi ya kilimo ni kazi ngumu mno na inachukua muda mrefu.Mkulima anatumia nguvu nyingi na rasmali fedha.Lakini anachopata wakati wa kuuza,hakirudishi gharama iliyotumika.Ni wakati sasa mamlaka zinazohusika kuangalia namna ya kumsaidia mkulima, aanze kunufaika na mazao yake ikiwemo alizeti”,amesema Mwakabuta.

Pia,meneja huyo amependekeza kuanzishwa kwa mashamba darasa yaliyolimwa kisasa na kupandwa mbegu bora,ili wakulima waweze kujifunza na kuiga kilimo hicho.

Katika hatua nyingine,mkulima na wakala wa kampuni ya Mount Meru,Mohammed labia,alisema kumekuwa na tabia ya kuagiza wakulima watumie mbegu bora,lakini ufuatiliaji wake ni duni.

“Ni kweli msimu wa mvua unapokaribia,mbegu bora inakuwa ni wimbo.Ufuatiliaji wake haufanyiki.Tatizo jingine kubwa ni kwamba mbegu bora nyingi bei yake ni kubwa mkulima wa kawaida hawezi kumudu kuzinunua.Naomba mamlaka zinazohusika,ziangalie uwezekano wa kupunguza bei.Au kuwepo na ruzuku katika mbegu bora”,amesema mkulima Labia.

Ameongeza kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kukutana na makampuni yanayozailisha mbegu bora kuweka bei itakayowavutia wakulima kukimbilia kununu mbegu hizo.Vile vile serikali isisitize uzalishaji wa mbegu bora na sio bora mbegu.

Kwa upande wa maafisa ugani,amewataka watoke maofisini na kuwa karibu na wakulima na kuwapa maelekezo na ushauri juu ya kilimo chenye tija.