Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
SERIKALI imewakaribisha wawekezaji katika kuongeza thamani ya mnyororo wa bidhaa za kilimo, ufugaji na uvuvi kwa kuwa mazingira ya uwekezaji ni rafiki.
Akizungumza katika kuitangaza Tanzania na vivutio vyake kwenye Jukwaa la Kilimo Biashara lililoandaliwa na Taasisi ya Jukwaa la Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRF) na kufanyika Kigali, Rwanda kwa njia ya video, Naibu Waziri wa Kilimo Omar Mgumba, amesema Tanzania ipo tayari kwa uwekezaji.
Naibu Waziri huyo amesema, pamoja na kuwezesha mazingira rafiki kuwa kisiwa cha amani, Serikali ya Tanzania imetengeneza miundombinu ambayo inawezesha wawekezaji kufikia soko la ndani na nje.
Pamoja na kuwa na uhakika wa umeme mpaka vijijini, serikali pia imeboresha miundombinu ya barabara kiasi cha mwekezaji kufika kokote anakotaka.
Katika mkutano huo wa kutambulisha Tanzania katika uchumi wa kilimo biashara, Mgumba amesema, pamoja na kuita wawekezaji katika mashamba makubwa ya miwa kwa ajili ya sukari na pamba kwa ajili ya kusokota nyuzi na kuuza mavazi, uvuvi wa kina kikuu, fursa zilizopo nchini katika kilimo, ufugaji na uvuvi zinaambatana na uwepo wa soko la ndani lenye wananchi takribani milioni 60, soko la Afrika Mashariki na soko la Kusini.
Amesema, wawekezaji hawatajutia uamuzi wao wa kuwekeza nchini kwa kuwa Tanzania tangu Uhuru ni nchi yenye amani na imethibitishwa na Global Peace Index kuwa Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika, ndiyo yenye amani uchumi wake unakua na ina raslimali tosha za asili kwa ajili ya kutumika kama malighafi.
“Tanzania ina zaidi ya hekta milioni saba za ardhi zinazofaa kulimwa zikiwa na uwezo wa kulima kwa umwagiliaji kutokana na kuzungukwa na mito na maziwa,” amesema Mgumba.
Amesema, lengo la serikali ni kuwa ifikapo mwaka 2025, Taifa linakuwa na uchumi wa kati, unawezesha kuwepo kwa mnyororo wa thamani kwa bidhaa za viwandani na hivyo kuinua ajira ya wakulima, ambayo ni asilimia 66 ya ajira nchini.
Amesema kuwa, serikali imefanya mabadiliko mengi katika sera, sheria na tozo ili kuwezesha uwekezaji kuwa rafiki zaidi na hasa uwekezaji wa uvuvi kina kikuu.
Naibu waziri huyo amesema, kuna mambo mengi ambayo yanatoa fursa ya uwekezaji na yameelezwa katika ASDP 11 sehemu ya tatu.
Katika mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Dkt. Maduhu Kazi amesema, Tanzania inawakaribisha wawekezaji na kwamba wapo tayari kuwahudumia.
Amesema, Taifa ni salama lenye amani likifuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na kwamba uchimi wake unakua na uko salama, kutokana na kuwa na utulivu muda wote hata wakati na baada ya uchaguzi.
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari