May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yajipanga uwekezaji wa teknolojia sekta ya madini

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam

SERIKALI imesema, inajipanga kuwekeza katika teknolojia ya utafiti, ili kusaidia kupata taarifa za kijiolojia zitakazowezesha kupata taarifa za kina katika sekta ya madini nchini.

Hali hiyo itasaidia kushawishi uwekezaji utakaoongeza kufunguliwa kwa migodi mingi itakayotengeneza ajira za kutosha.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, aliyekuwa mgeni rasmi, akimuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa tano wa Kimataifa wa Uwekezaji Sekta ya Madini, unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC).

Pia, Serikali imewataka wadau wa sekta ya madini kuwekeza katika uchenjuaji, utafutaji, uhifadhi na ufanyaji biashara ya madini kwa kuangalia maslahi ya nchi na watu wake.

Dkt. Biteko amesisitiza kuiwezesha migodi nchini, sambamba na wachimbaji wadogo ikiwemo katika upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa kuiunganishia na gridi ya umeme ya taifa.

“Migodi zaidi ya 350 imeunganishwa na gridi ya taifa ya umeme,” amesema Biteko kwa niaba ya Rais Samia.

Dtk. biteko ameongeza kuwa, Serikali itahakikisha inanunua mitambo mingi ili kusaidia wachimbaji wadogo.