December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yajidhatiti utekelezaji Programu ya BBT

Na Joyce Kasiki ,Dodoma

WAZIRI wa Kilimo Hussein Bashe amesema Serikali imeshapata  Dola Milioni 610  kati ya Dola Bilioni 1.8  kwa ajili ya kujenga mabwawa ,kuchimba  visima , na kufungua mashamba kwa ajili ya wakulima wadogo wakiwemo vijana wa Programu ya Serikali kwa Vijana ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) .

Waziri Bashe ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo ya Jeshi a Kujenga Taifa kundi Maalum KJ 834 Makutupora  BBT operesheni ya miaka 60 ya JKT huku akisema fedha hizo ni kwa ajili ya kunua matenki, vifaa vya umwagiliaji na vifaa mbalimbali ambavyo vitawasaidia katika uzalishaji wa kilimo wanachofanya.

“Kwa  hiyo Rais Samia Suluhu Hassan anafanya jitihada ambazo katika dola bilioni 1.8 zinazohitajika katika mradi wa kilimo kwa wakulima wadogo wakiwemo vijana wa BBT , mpaka sasa tumeshakusanya dola milioni  610 kwa ajii ya kujenga mabwawa,kuchimba visima na kufungua mashamba.”amesema Bashe

Aidha amesema,licha ya kuwepo kwa maswali ya kuondolewa kwa watakaokiuka masharti ya Mradi huo ,Serikali haitasiata kumwondoa yeyote kwa sababu Serikali inatumia fedha za umma katika kuhakikisha inakuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Hata hivyo Waziri huyo amesema,awamu ya pili ya BBT washiriki watakaochaguliwa wataanzia Makutupora kwa ajili ya kupata mafunzo ya kuwajengea uzalendo na uwapa ujuzi katika uzalishaji na uadilifu.

Akizungumza wakati akimkaribisha Waziri Bashe,Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele amewaasa vijana wa BBT waliomaliza mafunzo ya JKT kuwa raia wema , kuacha kujihusisha na migomo mbalimbali lakini pia kuwa mabalozi wazuri hasa wanapoenda kuanza shughuli zao za kilimo.

Meja Jenerali  Mabele amesema,fursa ya mafunzo hayo ni adimu na adhimu hivyo hawana budi kuyatumia kwa malengo yaliyokusudiwa na siyo vinginevyo.

Ametoa rai kwa taasisi nyingine kuona umuhimu wa mafunzo hayo ya Jeshi kwa ajili ya kuwajengea uzalendo ,uvumilivu na kupambana na changamoto za kimaisha .

Awali Kaimu Kamanda Kikosi 834 KJ Makutupora Meja James Macheta amesema wapo vijana watano  hawakuweza kumaliza mafunzo hayo kutokana na sababu mbalimbali huku wahitimu wa mafunzo wakiahidi kutumia ujuzi walioupata katika mafunzo hayo katika kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Muhitimu wa mafunzo ya JKT Asia Msuya amelishukuru Jeshi la Kujenga Taifa huku akisema mafunzo hayo ni nguzo muhimu katika kujenga umoja mshikamano na ari ya kulipenda Taifa lao.