December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaja na mpango wa kutokomeza malaria

Na Hadija Bagasha Tanga,

Serikali imeamua kuja na mpango wa kutokomeza ugonjwa wa malaria nchini ambao umekuwa ukisababisha vifo vingi vya watanzania kwa kuja na mpango maalumu wa upuliziaji wa dawa ya kuua mazalia ya mbu katika maeneo mbalimbali nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa wakati akifungua semina ya mafunzo ngazi ya Kata na Mtaa yanayohusu unyunyuziaji wa viuadudu vya kibaologia kwenye mazalio ya mbu waenezao Malaria.

Mgandilwa amesema kuwa serikali imeshapokea zaidi ya lita elfu 30 za dawa kwajili ya kufanya upuliziaji kwenye maeneo ambayo yanahisiwa kuwa na mazalia hayo ya viluilui vya mbu na kuwataka wananchi kuacha kuwa madaktari huko katika maeneo yao wakati upuliziaji huo ukiendelea ikiwa ni pamoja na kuacha kuhusisha dawa hizo na maswala ya kupunguza nguvu za kiume.

“Dawa hizi ni rafiki kwa wanyama isije kuaminishana mitaani kwamba kama mna ngombe zenu zitapoteza maisha kitendo ambacho si cha kweli tuwapeni ushirikiano wataalamu hawa wanapokuja kwenye maeneo yetu kwajili ya kufanya zoezi hili la upuliziaji wa dawa, “amesisitiza DC Mgandilwa.

Hata hivyo Mgandilwa ameitaka jamii kuacha tabia ya kuihusisha dawa ya kupulizia malaria kwamba inapunguza nguvu za kiume jambo si la kweli.

“Kuna watu mitaani wamekuwa wakijivika cheo cha udaktari serikali inakuja na mpango wa kuokoa maisha ya watanzania huku wengine wanapotosha watu kwamba dawa hazifai jambo hili tunapaswa kulikemea tunapoona wanatokea watu wachache mitaania wanaaminisha wenzao uongo tuwapinge, “amesititiza Mgandilwa.

Akizungumza katika mafunzo hayo mtaalamu wa afya ya jamii ambaye ni mratibu wa afya ya udhibiti wa viluilui vya mbu kutoka wizara ya afya Jubilete Bernard amemtaka kila mmoja kwenye nafasi yake kuhakikisha kwamba wanasimamia zoezi hilo kwa umakini ili kuweza kuleta tija kwa jamii ili kuepukana na mazalia ya viluilui vya mbu.

Amesema pamoja na kutoa mafunzo hayo lakini pia wanatoa vifaa hivyo jamii inapaswa kutoa ushirikiano wao kwa kuhakikisha wanatunza vifaa hivyo ili viweze kudumu kwani vikiharibika watakosa huduma ikiwa ni pamoja na kupulizia dawa kama watakavyoelekezwa na wataalamu.

“Waelezeni wananchi katika mikutano yenu kwamba kuna zoezi linaendelea la upuliziaji wa dawa ili waweze kuwa na uelewa wa kutosha wakati zoeli hilo likiendelea, “amesisitiza

Naye Dokta Ogla Mushi ambaye ni mratibu wa malaria Mkoa Tanga amesema Mkoa wa Tanga umepewa kipaumbele kufanya zoezi hilo katika halmashauri 3 Tanga Jiji, Lushoto na Handeni kama kianzio katika kufadhiliwa ambapo ameahidi mkoa wa Tanga kufanya vizuri.

“Lengo ni kupunguza ugonjwa wa malaria katika mkoa wa Tanga na kutokomeza ambapo kwa sasa maambukizi yapo asilimia 3.1 tunaamini ifikapo 2030 iwe chini ya asilimia 0 na ugonjwa huo uwe umetokomezwa kabisa, “amesisitiza Mushi.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Mohamed Kalua na Salim Lima wameahidi kusimamia vyema zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi ya kwamba dawa hizo hazina madhara hivyo wananchi waache kupotoshana.

Takwimu zinaeleza kuwa watanzania wengi wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa wa malaria hali iliyoilazimu serikali kuja na mpango wa kuutokomeza ugonjwa huo kwa kufanya upuliziaji wa dawa ili kuua mazalia ya mbu katika maeneo mbalimbali nchini lengo likiwa ni kutokomeza ugonjwa huo na kuokoa maisha ya watanzania.