Na Irene Clemence,Timesmajira
SERIKALI imeandaa mpango maalum wa kukuza viwanda nchini unaolenga kuimarisha uchumi wa viwanda na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania, hususan vijana.
Hayo yamebainishwa Jijini Dar es salaam mapema leo Desemba 18,2025 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga wakati akizugumza na waandishi wa habari kuhusu fursa za ajira zitakazopatikana kutokana na uwekezaji katika Viwanda na Biashara hususani kwa vijana
Amesema mpango huo unatarajiwa kuanzisha, kufufua na kuendeleza jumla ya viwanda 9,048 katika kipindi cha miaka sita, hatua itakayowezesha kupatikana kwa ajira takribani milioni sita nchini.

Amesema Katika utekelezaji wa mpango huo, Serikali imepanga kujenga kongani za viwanda katika mikoa yote ya Tanzania Bara, kwa kuzingatia fursa za kiuchumi na rasilimali zinazopatikana katika kila mkoa.

“Ujenzi wa kongani hizi unalenga kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji wa viwanda, kuongeza tija na kuharakisha maendeleo ya sekta ya viwanda” amesema
Amesema mpango huo ni fursa muhimu kwa vijana kushiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa thamani, kuanzia uzalishaji, uchakataji hadi masoko, hivyo kuchochea ajira, ujuzi na ujasiriamali wa viwanda.

Aidha amesisitiza kuwa utekelezaji wa mpango huo utaongeza kasi ya maendeleo ya viwanda, kukuza ajira na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako