November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaweka mkakati madhubuti kuinua uchumi kupitia gesi asilia

Na Agnes Alcardo, Timesmajira online, Dar es Salaam

SERIKALI inatarajia kutumia kiasi cha Trilioni 97 ambayo ni sawa na dola za kimarekani bil 47, ambazo zitatumika katika mradi wa kusafirisha gesi asilia kupitia kampuni mbalimbali zilizopo ndani na nje ya nchi.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar-es-Salaam kwenye maonesho ya 47 ya biashara ya Kimataifa, maarufu kama Sabasaba yanayoendelea kwenye viwanja vya Sabasaba na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Charles Sangweni.

Ambapo amesema mradi huo ukikamilika utaweza kuongeza uchumi wa nchi kuimarika zaidi tofauti na iliyokuwa awali.

” Sasa hivi tunajua kuwa uchumi wetu bado haujawa imara kama vile tunavyotegemea wengi wetu lakini kupitia mradi huo wa gesi utaenda kuwa mkombozi wa kuinua uchumi wa nchi,hivyo ushirikiano unahitajika baina ya serikali, wadau wa gesi na wananchi,” anasema Sangweni.

Katika hatua nyingine anasema mradi huo wa gesi unaoanzia Mnazi bay mkoani Mtwara, unatarajia kuanza hivi karibuni katika maeneo yaliyotengwa ambayo litapita bomba hilo na utatoa ajira kwa vijana wa kitanzania zaidi ya elfu kumi.

Aidha kwa upande wa visima vya mafuta, amesema hadi sasa serikali imefanikiwa kuchimba visima 96 kati ya hivyo 44 vimegundulika kuwa na mafuta huku visima 52 vikiwa havina kitu, hiyo ni kutokana na utafiti uliofanywa na mamlaka hiyo mwaka 2010-2012 katika maeneo mbalimbali nchini.

Pia anaongeza kuwa, PURA itaendelea na usimamizi na udhibiti wa shughuli za uzalishaji na utafutaji gesi asilia, ili kuhakikisha shughuli hizo zinafanywa kwa mujibu wa sheria.