November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaitaka OSHA kutathmini maeneo ya kazi

Na Bakari Lulela,Timesmajira Online.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama ameuagiza Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), kutathmini maeneo ya kazi yanayoongoza kwa matukio ya ajali na magonjwa pamoja na kubainisha visababishi vyake, ili kuwezesha uandaaji wa mkakati wa kudhibiti visababishi hivyo.

Ametoa agizo hilo alipokuwa akifungua kikao cha pili cha Baraza la Wafanyakazi wa OSHA, kilichofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kupitia bajeti ya mwaka 2021/22.

“Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mtendaji Mkuu, inaonesha taasisi yenu imekuwa na mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ambayo yametokana na maboresho mbalimbali yaliyokuwa yakifanyika na serikali ikiwemo kuondoa baadhi ya tozo ambazo zilionekana kuwa kero.

“Nawaagiza kuendelea kufanya kazi kwa weledi na uadilifu, ili kuweza kufikia lengo letu la kupunguza ajali na magonjwa yatokanayo na kazi na kuleta ustawi wa taifa letu,” amesema.

Waziri huyo amewashauri wajumbe wa kikao hicho, kufanya majadiliano katika kikao hicho kwa hekima na busara na hatimaye kutoka na maazimio muhimu, ambayo yatafanyiwa kazi ili kutimiza malengo ya taasisi.

Ameitaka OSHA, kuendeleza kubuni mifumo mbalimbali ya Tehama ambayo itaboresha utoaji wa huduma kwa wadau pamoja na kuweka taratibu za huduma, ambazo ni rafiki kwa wadau ili kuendana na maelekezo ya serikali.

Awali wakati akimkaribisha Waziri ambaye alikuwa mgeni katika kikao hicho Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema maboresho ambayo yamekuwa yakifanyika na serikali katika sekta ya biashara na uwekezaji, ikiwemo kuondoa baadhi ya tozo yamesababisha taasisi hiyo kupata mafanikio makubwa.

Kwa upande wake mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Taifa, Fidelis Athumani na mjumbe wa baraza hilo Joyce Mwambungu, wameipongeza serikali na uongozi wa OSHA kwa maboresho ya utendaji, ambayo yamekuwa yakifanyika kutokana na ushirikishwaji wa watumishi kupitia vikao vya mara kwa mara vya Baraza la Wafanyakazi.

Kikao hicho ambacho ni cha pili cha Baraza la nne la wafanyakazi wa OSHA, pamoja na masuala mengine kilikuwa na ajenda kuu ya kupitia bajeti ya mwaka wa fedha ujao 2021/22.