December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaipatia Wizara ya Ardhi sh.bilioni 50 kuzikopesha Halmashauri 55

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WIZARA ya Fedha na Mipango  imetiliana saini hati ya makubaliano na Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi huku Wizara ya Fedha na Mipango ikiipatia  Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi shilingi bilioni 50 kwa ajili ya kuzikopesha Halmashauri 55 ili  kutekeleza Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi nchini.

Hafla ya utiaji Saini wa hati hiyo ya  makubaliano ya fedha hizo imefanyika Jijini Dodoma kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba , Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  William Lukuvi  na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Ummy Mwalimu.

Kufuatia hati hiyo ya makubaliano,Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Mwigulu Nchemba  ameziagiza  Halmashauri zote zilizopata fedha hizo  kuzitumia kwa kufuata Sheria,miongozo,na maelekezo yaliyowekwa ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa na kuwa mfano bora kwa wengine wanaohitaji.

Dkt.Nchemba amesema, utekelezaji wa programu hiyo ni muhimu kwa Serikali hususani Wizara ya Fedha kwa kuwa utatengeneza chanzo kipya cha kodi kwa miaka ijayo.

Amesema,mpango huo utaipeleka nchi katika hatua kubwa zaidi, lakini pia kuimarisha shughuli za uzalishaji kwa kutumia ardhi pamoja na kutatua migogoro ya ardhi ambayo imekuwa kero kwa muda mrefu.

Kwa Upande Waziri Ummy ameipongeza Serikali kwa hatua hiyo ambayo itawezesha utekelezaji wa kipaumbele cha wizara hiyo cha kuendeleza miji na vijiji huku akiahidi kuzisimamia fedha hizo kwa kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na siyo vinginevyo.

“Kimsingi naipongeza Serikali kwa hatua hii kubwa,niseme tu kwamba Wizara yangu inakwenda kuzisimamia fedha hizi na kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili nchi iweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.“amesema Waziri Ummy

Aidha amesema programu hiyo italeta matokeo chanya kwa kupunguza uendelezaji na ukuaji holela wa miji, kupendezesha mitaa na kuwa safi na salama pamoja na kuongeza maeneo ya ardhi kwa ajili ya miundombinu ya kijamii na kiuchumi

Naye Waziri Lukuvi amesema fedha hizo zitaziwezesha Halmashauri kiuchumi na kupata faida ya takribani shilingi bilioni 41 ndani ya miezi sita.

“Pamoja na kuziwezesha halmashauri, fedha hizo pia zitatumika kutatua kero na dhuluma kwa wananchi na kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwa wamiliki wa maeneo yaliyopimwa na kupangwa ni rahisi kukopesha kuliko wanaomiliki maeneo yasiyo rasmi.”amesema Lukuvi

Aidha Lukuvi ametumia nafasi hiyo kuwaagiza Wakurugenzi wote wanaopata fedha hizo kutatua changamoto mbalimbali za fidia kwa wananchi wanaochukuliwa ardhi na kuwataka kuhakikisha wanatumia fedha hizo kuwalipa wananchi fidia kabla ya kuchukua maeneo yao.

Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanueli Tutuba amesema utoaji wa fedha hizo ni utekelezaji wa majukumu ya wizara na kubainisha kuwa miongoni mwa majukumu ya msingi ya Wizara ya Fedha na Mipango ni kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kutekeleza mipango ya Serikali inayowezesha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, kuimarisha shughuli za uchumi na ustawi wa jamii, pamoja na kusimamia matumizi bora ya fedha za umma.

Fedha hizo zimetolewa kwa Halmashauri 55 zilizokidhi vigezo kati ya 78 zilipeleka mapendekezo, zilizopata fedha hizo ni pamoja na Dodoma Jiji shilingi bilioni tatu, Ilemela shilingi bilioni 3.5, Chalinze shilingi bilioni mbili na Meru shilingi bilioni 6.5.