Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma
MBUNGE wa Viti Maalum, Yumna Omar, amehoji Serikali kuhusu mikakati iliyowekwa kuhakikisha Tanzania inapata medali katika mashindano ya kimataifa ya michezo kwa watu wenye ulemavu (Paralympic Games), baada ya nchi kushiriki mashindano hayo tangu mwaka 1992 bila kupata medali yoyote.
Yumna aliuliza swali hilo leo Juni 25,2026 Bungeni jijini Dodoma wakati wa kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu bungeni jijini Dodoma, akitaka kufahamu hatua zinazochukuliwa na Serikali ili kuimarisha ushindani wa wanamichezo wenye ulemavu na kuwezesha Tanzania kupata mafanikio makubwa zaidi katika mashindano ya kimataifa.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira bora yatakayowezesha wanamichezo wenye ulemavu kufanya vizuri na hatimaye kuiletea nchi medali katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Amesema miongoni mwa hatua zinazochukuliwa ni kuimarisha miundombinu ya michezo ili kuwapa wanamichezo hao fursa nzuri za kujiandaa kabla ya kushiriki mashindano makubwa.
“Serikali itaendelea kutengeneza mazingira yatakayowezesha kupata medali hizo, ikiwemo kuandaa miundombinu bora ya michezo itakayowasaidia wanamichezo wetu wenye ulemavu kujiandaa kikamilifu wanapokuwa na mashindano. Miundombinu ni sehemu muhimu ya maandalizi ya kufanya vizuri,” amesema Dkt. Nchemba.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali itaendelea kusajili na kuziimarisha timu za michezo za watu wenye ulemavu ili kuongeza idadi ya wachezaji na kuwapatia vifaa na vitendea kazi vinavyohitajika kwa maendeleo ya michezo hiyo.
Amesema katika bajeti ya Serikali, juhudi zimeendelea kufanyika za kuweka mazingira bora ya uwezeshaji kwa timu za taifa, ikiwemo timu za watu wenye ulemavu, ili ziweze kushindana kwa kiwango cha juu zaidi.
Waziri Mkuu ameasisitiza kuwa licha ya Tanzania kutopata medali nyingi katika baadhi ya mashindano ya kimataifa, wanamichezo wenye ulemavu wameendelea kuiletea nchi heshima kubwa kupitia ushiriki wao na mafanikio mbalimbali katika medani za kimataifa.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa michezo kuhakikisha vipaji vya watu wenye ulemavu vinatambuliwa, vinaendelezwa na vinapewa fursa ya kushindana katika mashindano ya ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuongeza ushindani na mafanikio ya Tanzania kimataifa.

More Stories
REA Zambia yapongeza ubora wa miradi ya Umeme vijijini Tanzania
Serikali yazitaka taasisi kujiandaa kukabiliana na El Nino
NaCoNCO yapewa Dira kuimarisha maadili na uwajibikaji