December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Adam Nyaruhuma (aliyesimama) mmoja kati ya watoa mada katika mafunzo maalum yanayoendelea katika ukumbi wa Chuo Cha Utumishi wa Umma Mkoani Tabora akitoa elimu kwa Wathamini waliohudhuria mafunzo hayo kwa ajili ya usajili wa taaluma yao.

Serikali yaibana taaluma ya uthamini, vigezo maalum kutumika

Na Eliafile Solla, TimesMajira Online,Tabora

NENO uthamini linatokana na mzizi mkuu ambao ni thamani na hivyo kutengeneza tafsiri ya uthamini kuwa ni utaratibu na utaalam wa kukadiria, kushauri kuhusu thamani ya mali isiyohamishika kama vile ardhi,majengo ama mazao ya muda mrefu na muda mfupi.

Wataalam mbalimbali wa fani ya Uthamini wakiendelea na mafunzo maalum kwenye ukumbi wa Chuo Cha Utumishi wa Umma Mkoani Tabora kwa ajili ya kujengewa uwezo na usajili wa taaluma yao

Akizungumza na wathamini kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania katika kikao maalum mkoani Tabora Kaimu Msajili wa Bodi ya Wathamini Bw. Joseph Shewio amesema, thamani kwa ujumla wake inaweza kuelezeka kama bei inayolipwa kwa ajili ya kupata kitu lakini kwa lugha ya kitaaluma thamani hususan ya mali isiyohamishika inahusisha upatikanaji wake (availability, ubora wa matumizi yake (utility), mahali ilipo (location), umiliki wake (ownership).

‘‘Sisi kama wataalam ni lazima tujue kwa kina hizi tofauti ili wakati wa kutekeleza majukumu yetu tuzingatie vigezo na tusimamie miongozo inayotuongoza maana Serikali inatuamini hasa katika kusimamia weledi wa kufanya kazi za uthamini, amesema Shewio’’

Shewio ameongeza kwamba, Bodi ya Usajili wa Wathamini inatekeleza mpango maalum wa usajili wa Wathamini kote nchini kwa sababu, kwa muda mrefu Wathamini wengi walikuwa hawasajiliwi kutokana na changamoto za kisheria zilizokuwepo hapo awali.

Aidha, amedokeza kuwa tangu kuzinduliwa kwa Bodi ya Wathamini na Waziri mwenye dhamana ya Ardhi Mhe. William Lukuvi January 2018 Bodi imekuwa inatekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa katika Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini Sura 138 ya mwaka 2016 ambapo moja ya majukumu ya Bodi ni kuendesha mafunzo ya Wataalam wa Uthamini na kuwasajili kwa ajili ya kutoa huduma za Uthamini wa mali kwa Serikali na Umma.

“Miongozo yetu iko wazi na imetaja mali zinazothaminiwa ni pamoja na ardhi, nyumba, mashamba, mitambo na mashine, biashara, majengo, magari, mifugo, aina zote za uwekekezaji na kwamba uthamini unafanyika pale ambapo thamani ya mali husika inahitajika kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuweka mali rehani ili kupata mkopo, kuwekea mali bima, kulipa fidia ya mali, kuweka vizuri taarifa za mahesabu ya taasisi au biashara, kubadilishana mali, kuuza au kununua mali au kutoa zawadi ya mali” amesema Shewio’’.

Mpango huu wa kusajilil Wathamini unatekelezwa kwa awamu mbili kila mwaka ambapo awamu ya kwanza ilifanyika kuanzia Januari hadi Juni 2021 kwa kuhusisha mafunzo ya Wathamini 91 na sasa utekelezaji unaendelea katika awamu ya pili na usajili umeanza rasmi tangu mwezi Julai 2021 mafunzo yakihusisha Wataalam wa Uthamini 62 kutoka Ofisi za Serikali Kuu, Halmashauri, Taasisi za Umma na binafsi nchini Tanzania.