November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yahimiza vijana kuchangamkia fursa sekta ya mifugo,uvuvi

Na Mbaraka Kambona,TimesMajira Online,Dar

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega amewahimiza vijana kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta za mifugo na uvuvi ili waweze kuzitumia kujikomboa kimaisha.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia) akiangalia moja ya mbegu za malisho aina ya Juncao zinazozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa

Ulega amesema hayo alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo katika Monesho ya 45 ya biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam juzi.

Akiwa katika maonesho hayo amesema kuwa vijana watumie nafasi hiyo ya maonesho kwenda kujifunza fursa mbalimbali za kibiashara na za uwekezaji zinazopatikana katika sekta za mifugo na uvuvi kwa sababu wizara ya mifugo na uvuvi mambo yake mengi ni ya uzalishaji na biashara.

“Kila kitu kilichopo katika wizara hii ni fursa katika biashara na ni fursa ya uwekezaji, hivyo tunawashauri vijana kutumia fursa hii ya maonesho kujifunza na kutumia elimu watakayoipata kuboresha maisha yao huko wanakoishi,” amesema Ulega.

Ameendelea kusema kuwa katika banda la wizara hiyo kuna wataalam mbalimbali ambao wanatoa elimu na mafunzo yanayohusu ufugaji, hivyo wakifika hapo watajifunza namna ya kufuga kuku, ng’ombe, mbuzi au Samaki kibiashara.

Ameongeza kuwa kuna vijana wengi wanaotafuta kazi lakini bado hawajafanikiwa, hivyo aliwashauri kwenda kujifunza fursa kubwa za kibiashara zitakazowasaidia kujipatia ajira na kukuza uchumi wa nchi pia.

“Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan imejikita katika kufungua milango ya biashara, kwa hivyo, hivi sasa wale wote wenye kiu ya kujifunza na kufanya kazi ya uzalishaji tunawakaribisha hapa ili waweze kufanya kazi hiyo ambayo itakuwa na manufaa sio kwao tu bali kwa taifa pia,’’ameongeza Ulega.

Katika hatua nyingine,Waziri Ulega amezitaka taasisi zilizo chini ya wizara hiyo ikiwemo Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) na Wakala ya Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kubuni mafunzo yatakayojumuisha watu wa elimu ya chini kabisa ambao wengi wao ni darasa la saba.

Alisema kwa sasa vijana wengi ambao hawajasoma wanakimbilia katika kuendesha bodaboda kwa maana ndio njia wanayoiona rahisi ya kujipatia kipato huku akizitaka taasisi hizo kuja na mkakati maalum wa kuanzisha mafunzo ya kuwafundisha vijana hao fursa mbalimbali zilizopo katika sekta hizo mbili na wakazitumia kujiajiri na kufanya uzalishaji mkubwa utakaowezesha hata nchi kupata mapato.