November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yahimiza nguvu uchumi wa kidigitali kwa wanawake, vijana

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KWA kuwa wanawake na vijana ni msingi na chachu ya mabadiliko wa masuala yote ya kiuchumi na kijamii, serikali imetaka wadau wote kushirikiana kuwezesha makundi hayo kuchangamkia fursa zinazoambatana na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Aidha imesisitizwa kwamba kundi hilo lenye nafasi ya kipekee katika kuelimisha umma juu ya teknolojia mpya za kidijitali, matumizi salama na yenye tija ya TEHAMA ili kuwesha uchumi wa kidijitali ulio shirikishi, yaani “inclusive digital economy” ni lazima liandaliwe kuwa na kasi ya matumizi ya Teknolojia za kidijitali.

Kauli hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari Selestine Kakele akifungua Mkutano wa wanawake kwenye Kongamano la Saba la Tehama Tanzania jana lililoandaliwa na Tume ya Tehama chini ya uongozi wa Dkt Nkundwe Mwasaga.

“Serikali, kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inapenda kuwashukuru wadau wote wa maendeleo ya TEHAMA katika kulitambua kundi hili muhimu na kuendelea kuwezesha wanawake na vijana kuchangamkia fursa zinazoambatana na TEHAMA. “ amesema.

Amesema serikali imeweka mazingira rafiki ya kukuza na kuibua ubunifu, kuchochea uwekezaji na uendelezaji wa Teknolojia za kisasa na TEHEMA kwa kutunga na kusimamia utekelezaji wa sera, sheria, kanuni na taratibu pamoja na miongozo mbalimbali.


Aidha amesema nguzo ya uchumi jumuishi wa kidigitali, inakusudia kupunguza na hatimae kuondoa kabisa pengo baina ya watu wanaofikia na kutumia huduma za kidigitali na wasiopata fursa hiyo (digital divide).

Aidha, nguzo hii inaweka msingi wa kushughulikia vikwazo vya kupata fursa ya kupata elimu na mafunzo ya TEHAMA kwa jamii. Lengo ni kuhakikisha kwamba kila mtu pasipokujali hali yake au sehemu anayotoka anashiriki na kufaidika na uchumi wa kidigitali.

“Mtakubaliana nami kwamba ili maendeleo yaweze kuwa na maana hayana budi kufangamanishwa moja kwa moja na watu. Aidha, kigezo muhimu cha watu, ni kufikiwa kwa makundi yote katika jamii pasipo ubaguzi wa aina yoyote. Katika muktadha huu, ili kujenga msingi wa maendeleo endelevu, matumizi ya TEHAMA kama nyenzo wezeshi hayana budi kufikia makundi yote katika jamii.” amesema.

Naibu Katibu mkuu huyo alitoa rai kwa wanawake kutumia jukwaa hili na fursa hii, kupaza sauti zao na kupitia sauti hizo kama taifa tuweze kujadiliana kuhusu vikwazo vinavyowakabili wanawake na kufanya washindwe kuchangamkia matumizi ya Teknolojia na TEHAMA kwa ujumla katika shughuli zao za kila siku.

Aidha katika matumizi hayo amesema kwamba wanawake na vijana wana nafasi maalumu ya kuongoza harakati za kupinga matumizi mabaya ya TEHAMA.

“Sisi kama Wizara yenye dhamana ya TEHEMA hapa nchini, tungependa kusikia sauti zenu, mkielezea fursa zilizopo na changamoto za matumizi ya TEHEMA. Aidha, tutafurahi kusikia kuhusu mawazo yenu, maoni yenu na matarajio yenu kwa serikali juu ya nini kifanyike ili kuendelea kujenga mazingira mazuri na rafiki kwa wanawake kufikia na kutumia teknolojia zinazoibukia,” amesema.

Nguzo ya uchumi jumuishi wa kidigitali, inakusudia kupunguza na hatimae kuondoa kabisa pengo baina ya watu wanaofikia na kutumia huduma za kidigitali na wasiopata fursa hiyo (digital divide).

Aidha, nguzo hii inaweka msingi wa kushughulikia vikwazo vya kupata fursa ya kupata elimu na mafunzo ya TEHAMA kwa jamii. Lengo ni kuhakikisha kwamba kila mtu pasipokujali hali yake au sehemu anayotoka anashiriki na kufaidika na uchumi wa kidigitali.

“Wakati tukiendelea kuweka mazingira mazuri kwa ukuaji wa TEHAMA nchini, ni vema tukashirikiana pamoja kutatua changamoto zinajitokeza kwa wakati. Tuhakikishe tunatoa elimu kwa umma juu ya matumizi salama ya TEHAMA pamoja na kujikinga na matumizi mabaya ya TEHAMA ili kujipatia maendeleo. “ amesema.

Naibu Katibu Mkuu wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Selestine Kakele (katikati) akifuatilia mada mbalimbali katika siku ya kwanza ya Kongamano la Tehama iliyogusa zaidi wanawake na vijana. Anayefuatia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Tehama, Profesa Leonard Mselle na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Dkt. NKUNDWE MWASAGA jana kwenye Ukumbi wa JNICC, Dar es Salaam. Kongamano hilo linatarajiwa kufunguliwa rasmi leo na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, NAPE NNAUYE